DIRISHA la usajili bado halijafunguliwa, lakini kwa kuwa tayari msimu wa 2015/16 unakwenda ukingoni, kuna mengi yanaanza kusikika kipindi hiki kuhusu usajili hasa kwa kuwa wachezaji wengi wanaelekea ukingoni mwa mikataba yao.
Kila mchezaji ana malengo yake kutokana na jinsi anavyokiona kiwango na nafasi yake kwenye timu.
Klabu nyingi katika nchi zilizoendelea au zenye viwango vizuri vya soka ni kawaida kwa uongozi wa klabu kuwahi kumuongezea mkataba tofauti na hapa nchini ambapo kuna wachezaji wengi tu wenye umuhimu kikosini wamekuwa wakienda mpaka mwisho wa mikataba yao bila kuongezewa mipya.
Mfano mwepesi ni jinsi ilivyokuwa kwa Gareth Bale, alipokuwa Tottenham Hotspur alisainishwa mkataba mpya kabla ya ule wa awali kumalizika kwa kuwa matajiri wa Real Madrid walishaanza kumnyatia, hivyo hata aliposajiliwa thamani yake ikawa juu tofauti na tofauti na kama angesajiliwa akiwa mwishoni mwa mkataba wake, thamani ingepungua.
Upande wa Tanzania wachezaji wengi nao wameonekana kuamka wakitaka kusajiliwa kwa dau kubwa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Hamasa hiyo imetokana na klabu za Tanzania kusajili wachezaji wa nje kwa fedha nyingi, mfano Thabani Kamusoko na Donald Ngoma waliotua Yanga wakitokea FC Platinum ya Zimbabwe, Ngoma alisajiliwa kwa zaidi ya shilingi milioni 100, Kamusoko kwa zaidi ya shilingi milioni 80.
Miezi ya hivi karibuni imekuwa ni jambo la kawaida kusikia wachezaji wazawa hasa wale wenye majina makubwa wakitaja madau yao ya usajili kuanzia shilingi milioni 50 au 60 au zaidi ya hapo, hawa ni baadhi yao.
Singano Kiungo wa Azam FC, Ramadhan Singano ‘Messi’, aliingia kwenye mgogoro mkubwa na klabu yake ya zamani ya Simba ambapo alidai mkataba umeisha na hajatimiziwa mahitaji yake ya kimkataba.
Simba walitaka asaini kwa miaka miwili huku wakimuwekea dau la milioni 30 na mshahara wa milioni 1.5, Messi alikataa na kutaka apewe milioni 60, hata alipobembelezwa alishikilia msimamo wake japokuwa baadaye alishusha na kutaka apewe milioni 50, lakini Simba wakawa wagumu kutoa kiwango hicho pia.
Baada ya ishu ya mgogoro wake na Simba kuwa kubwa na hatimaye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likaidhinisha mchezaji huyo kuwa huru, Azam ikatumia mwanya huo kumdaka na kumpa mkataba wa miaka mitatu.
Julai, mwaka jana ndiyo Messi alijiunga na Azam ambapo iliripotiwa kwamba alipewa dau la milioni 50, huku mshahara wake ukiwa ni milioni mbili kwa mwezi. Mkude KIUNGO wa Simba, Jonas Gerald Mkude, Novemba, mwaka jana aliongeza mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kuitumikia klabu yake ya Simba baada ya ule wa awali kumalizika.
Kabla ya kuingia mkataba huo mpya, Mkude alikuwa kwenye mvutano na viongozi wake juu ya makubaliano ya kimslahi, lakini mwisho wa siku mambo yakenda sawa na mpaka leo bado kiungo huyo anaitumikia Simba na mara kadhaa amekuwa akivaa kitambaa cha unahodha kwenye mechi mbalimbali za Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
Kama ilivyo kwa wengine, naye Mkude hajasaini mkataba huo kwa urahisi mpaka alipopewa milioni 60 pamoja na gari aina ya Toyota Mark II Grand.
Ndemla baada ya kuona Mkude amepewa alichotaka, kwa kuwa Ndemla na Mkude wamekua pamoja, naye akaanza kudai kiasi cha fedha kama cha Mkude, mvutano ukaanza lakini baadaye viongozi wa Simba wakamuwahi na kumsomesha, akakubali kupokea shilingi milioni 40, akasaini kuendelea kuichezea Simba.
Kessy Kabla ya beki wa kulia, Hassan Kessy hajajiunga na Simba katikati ya msimu wa 2014/15 akitokea Mtibwa Sugar, kwanza alikuwa akigombaniwa na timu za Simba na Yanga huku mwenyewe akihitaji apewe si chini ya milioni 50 ndiyo ajiunge na moja ya klabu hizo.
Mwisho wa siku akatua Simba na kupewa mkataba wa mwaka mmoja na nusu huku ikiripotiwa alisajiliwa kwa dau la Sh milioni 30.
Baada ya kutua Simba akaitumikia kwa kiwango cha hali ya juu kiasi kwamba hata Yanga wakaanza kumfukuzia baada ya mkataba wake wa sasa kuelekea ukingoni. Kuona kwamba kiwango chake ni mali, Kessy amewaambia Simba wampe milioni 60 ndiyo akubali kuanguka saini kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Yondani Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), hali ilivyo kwa sasa beki tegemeo wa Yanga, Kelvin Yondani, anaruhusiwa kuanza mazungumzo na klabu yoyote itakayomuhitaji baada ya mkataba wake kubaki miezi miwili kabla ya kumalizika.
Kabla hajazipa nafasi klabu zingine, tayari amewaambia mabosi wake kwamba anataka kubaki kuendelea kukipiga klabuni hapo lakini amesisitiza anataka awekewe mezani kitita cha Sh milioni 60 ili asaini mkataba mpya.
Beki huyo ambaye ni kipenzi cha Mholanzi, Hans van Der Pluijm, alijiunga na Yanga msimu wa 2011/2012 akitokea Simba baada ya mkataba wake kumalizika na iliripotiwa kwamba alipewa Sh. milioni 30 akaamua kumwaga wino Jangwani.
www.mdosejr@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni