RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi jana alilazimika kusitisha kwa muda zoezi la kusalimiana na wacheaji ili kuzungumza na Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kumsihi aitikie wito wa kocha Charles Boniface Mkwasa timu ya taifa.
Malinzi aliyekuwa mgeni rasmi katika fainali ya Kombe la TFF, maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC), kati ya Azam na Yanga iliyoshinda 3-1 jana, alisimama kwa sekunde kadhaa kumnong’oneza Cannavaro.
Kama ilivyokuwa hisia za wengi – kwamba anambembeleza Cannavaro aitikie wito wa Mkwasa Stars, na ndivyo ilivyokuwa.
Cananavaro alisema jana baada ya mechi kwamba Rais Malinzi alimsihi aende Taifa Stars.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi (kulia) akizungumza na Cannavaro jana Uwanja wa Taifa
“Mimi sitajiunga na timu, nimemsikia Rais, nitakwenda kwa kocha (Mkwasa) na kumueleza rasmi uamuzi wangu wa kustaafu Taifa Stars,”amesema Cannavaro.
Beki huyo wa kati amesema kitendo alichofanyiwa na Mkwasa si cha kiungwana kumvua Unahodha wa Taifa Stars kupitia vyombo vya Habari yeye akiwa majeruhi, hivyo ameona bora astaafu tu.
Mapema mwaka huu, Mkwasa alimtangaza mshambuliaji wa KRC Genk, Mbwana Samatta kuwa Nahodha mpya wa Taifa Stars badala ya Cannavaro.
Na Mkwasa alisema alifikia uamuzi huo, baada ya Samatta kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika akiwa TP Mazembe aliyoshinda nayo taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kuhamia Genk.
Mkwasa alisema amempa Unahodha Samatta ili kumhamasisha ahamishie mafanikio ya klabu katika timu ya taifa.
Malinzi pia alipata fursa ya kuzungumza na Cannavaro wakati anakabidhi zawadi za ushindi wa Yanga |
Lakini kosa la wazi, Mkwasa hakukutana na Cannavaro kujadili naye kabla na kwa sababu hiyo Mzanzibari huyo amesusa Taifa Stars.
Mkwasa ametaja kikosi cha Stars kitakachocheza na Kenya Mei 29 mjini Nairobi ndani yake akimjumuisha Cannavaro na kumrejesha kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, akimtema Ally Mustafa ‘Barthez’, wote wa Yanga.
Kikosi kamili alichotaja Mkwasa kinaundwa na makipa; Deo Munishi ‘Dida’ (Yanga SC), Aishi Manula (Azam FC), Beno Kakolanya (Prisons FC).
Mabeki; Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga SC), Aggrey Morris (Azam FC), Erasto Nyoni (Azam FC), David Mwantika (Azam FC), Juma Abdul (Yanga SC), Mwinyi Hajji Mngwali (Yanga SC) na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba SC).
Viungo; Himid Mao (Azam Fc), Mohammed Ibrahim (Mtibwa Sugar), Shizza Kichuya (Mtibwa Sugar), Jonas Mkude (Simba SC), Ismail Issa Juma (JKT Ruvu), Mwinyi Kazimoto (Simba SC), Farid Mussa (Azam FC), Juma Mahadhi na Hassan Kabunda (Mwadui FC).
Washambuliaji Thomas Ulimwengu (TP Mazembe – DRC), Mbwana Samatta (KRC Genk – Ubelgiji), Elias Maguri (Stand United), Ibrahim Hajib (Simba SC), John Bocco (Azam FC), Deus Kaseke (Yanga SC) na Jeremiah Juma (Prisons).
Mchezo dhidi ya Kenya ni sehemu ya maandalizi kwa timu zote mbili kabla ya mechi za kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika mwezi ujao.
Taifa Stars inatarajiwa kuingia kambini leo kujiandaa na mchezo huo wa kirafiki kabla ya kuwakabili Misri katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Juni 4, mwaka huu.
PICHA NA BIN ZUBEIRY
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni