AZAM FC imeipiku Simba SC kwa kumaliza nafasi ya pili baada ya mechi za mwisho za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo.
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, JKT Ruvu imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba SC, mabao yake yakifungwa na Abdulrahman Mussa dakika ya kwanza na 30, wakati la Wekundu wa Msimbazi limefungwa na Nahodha Mussa Hassan Mgosi dakika ya 70.
Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam pia, wenyeji Azam FC wamelazimishwa sare ya 1-1 na Mgambo JKT ya Tanga.
Ramadhani Singano ‘Messi’ alianza kuifungia Azam FC dakika ya 60 kabla ya Fully Maganga kuisawazishaia Mgambo dakika ya 72.
Kiungo wa Simba, Abdi Banda akipambana katikati ya wachezaji wa JKT Ruvu leo |
Kwa matokeo hayo, Azam FC inamaliza na pointi 64, ikifuatiwa na Simba SC inayomaliza na pointi 62 katika nafasi ya tatu.
Yanga SC ambayo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu wiki mbili zilizopita, leo imemaliza kwa sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji Majimaji Uwanja wa Majimaji mjini Songea hivyo kufikisha pointi 73.
Mechi nyingine za kufunga pazia la Ligi Kuu, wenyeji Toto Africans wamefungwa 1-0 na Stand United Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Coastal Union wamefungwa 2-0 na Prisons
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Mbeya City imelazimishwa sare ya 0-0 na Ndanda FC, Mtibwa Sugar wameichapa 2-0 African Sport na Kagera Sugar wameshinda 2-0 dhidi ya Mwadui FC.
Kwa matokeo hayo, timu zote za Tanga, Mgambo JKT, African Sports na Coastal Union zinaipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu, zikizipisha Ruvu Shooting, Mbao FC na African Lyon.
Mgambo JKT imemaliza na pointi 28, African Sports 26 na Coastal 22.
ORODHA YA WAFUNGAJI BORA
Player | Goals | |
---|---|---|
1 | Amisi Tambwe | 21 |
2 | Hamisi Kiiza | 19 |
3 | Donald Ngoma | 17 |
4 | Elias Maguli | 13 |
5 | Jerema Juma | 13 |
MSIMAMO WA LIGI KUU YA VODACOM
Rn | Timu | P | W | D | L | F | A | Gd | Pts |
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
1 | YANGA | 30 | 22 | 7 | 1 | 70 | 20 | 50 | 73 |
2 | Azam FC | 30 | 18 | 10 | 2 | 47 | 24 | 23 | 64 |
3 | SIMBA SC | 30 | 19 | 5 | 6 | 45 | 17 | 28 | 62 |
4 | T. PRISONS | 30 | 13 | 12 | 5 | 28 | 22 | 6 | 51 |
5 | MTIBWA SUGAR | 30 | 14 | 8 | 8 | 33 | 21 | 12 | 50 |
6 | MWADUI FC | 30 | 11 | 8 | 11 | 29 | 29 | 0 | 41 |
7 | STAND UNITED | 30 | 12 | 4 | 14 | 28 | 30 | -2 | 40 |
8 | MBEYA CITY | 30 | 9 | 8 | 13 | 32 | 34 | -2 | 35 |
9 | NDANDA FC | 30 | 7 | 14 | 9 | 28 | 31 | -3 | 35 |
10 | MAJIMAJI FC | 30 | 9 | 8 | 13 | 22 | 40 | -18 | 35 |
11 | JKT RUVU | 30 | 8 | 8 | 14 | 31 | 39 | -8 | 32 |
12 | KAGERA SUGAR | 30 | 8 | 7 | 15 | 24 | 34 | -10 | 31 |
13 | TOTO AFRICANS | 30 | 7 | 9 | 14 | 26 | 40 | -14 | 30 |
14 | MGAMBO SHOOTING | 30 | 6 | 10 | 14 | 24 | 36 | -12 | 28 |
15 | AFRICAN SPORT | 30 | 7 | 5 | 18 | 13 | 34 | -21 | 26 |
16 | Coastal Union | 30 | 5 | 7 | 18 | 17 | 41 | -24 | 22 |
WAKATI HUO;
BEKI wa kulia, Juma Abdul Jaffar Mnyamani ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mwezi Aprili, 2016 baada ya kuwashinda kwa kura mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma anayecheza naye Yanga SC ya Dar es Salaam na kiungo Hassan Dilunga wa JKT Ruvu ya Pwani.
Katika rekodi za Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) iliyoketi Jumamosi Iliyopita, imeonesha kwamba Abdul alicheza mechi zote tano za Ligi Kuu kwa mwezi Aprili ambapo pia aliifungia timu yake bao katika harakati za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/16.
Juma Abdul Jaffar Mnyamani (kushoto) ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwezi Aprili |
Uwezo aliouonyesha Abdul ulisababisha Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kumjumuisha katika kikosi chake kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Harambee Stars ya Kenya kadhalika Mapharao wa Misri katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Juni 4, mwaka huu.
Wachezaji bora wa miezi minne iliyopita ni kiungo Thaban Kamusoko wa Yanga SC (Desemba 2015), beki Shomari Kapombe wa Azam (Januari 2016), Mshambuliaji Mohamed Mkopi wa Tanzania Prisons (Februari 2016) na Shiza Ramadhani Kichuya wa Mtibwa Sugar (Machi 2016).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni