TANZANIA imejitoa kuandaa michuano ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame mwaka 2016.
Rais
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema mapema leo kwamba
kujitoa kwako kumetokana na kubanwa na ratiba za mashindano mbalimbali ya
kimataifa kati ya Juni na Septemba.
“Shirikisho
la mpira wa miguu Tanzania halitaandaa mashindano ya CECAFA Kagame cup 2016.
Hii ni kutokana na muingiliano wa ratiba ya kimataifa,”amesema Malinzi katika
taarifa yake fupi kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini leo.
TFF ililikubalia Baraza la Vyama vya Soka Afrika
Mashariki na Kati (CECAFA) kuandaa kwa mara ya pili michuano ya Kombe la Kagame
mwaka huu, baada ya mwaka jana kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Katika
mashindano ya mwaka jana, Azam FC waliibuka mabingwa baada ya kuifunga Gor
Mahia ya Kenya katika fainali 2-0, mabao ya Nahodha, John Bocco dakika ya 17 na
Kipre Herman Tchetche dakika ya 64 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na
inaonekana wazi TFF imamua kuachana na Kombe la Kagame, baada ya timu yenye
mvuto zaidi wa mashabiki nchini, Yanga SC kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la
Shirikisho Afrika hivyo haitaweza kushiriki michuano hiyo ya CECAFA.
Na
inaonekana TFF inaona inahofia kupata hasara kufanya mashindano hayo bila ya
Yanga kushiriki – wakati huo huo inaonekana pia timu nyingine yenye mashabiki
wengi nchini, Simba SC haiko tayari.
Yanga
ambao ni mabingwa wa mataji yote matatu nchini msimu huu, Ngao ya Jamii, Kombe
la Ligi na Kombe la TFF maarufu kama ASFC, imepangwa Kundi A katika Kombe la
Shirikisho Afrika pamoja na mabingwa wa zamani barani, TP Mazembe ya DRC, MO
Bejaia ya Algeria na Medeama ya Ghana.
Kundi B linaundwa na timu za Kaskazini mwa Afrika tupu
ambazo ni Etoile du Sahel ya Tunisia ambao ni mabingwa watetezi, Ahly Tripoli
ya Libya, FUS Rabat na Kawkab zote za Morocco.
Yanga
watafungua dimba na Mouloudia Olympique Bejaia nchini Algeria Juni 17, mwaka
huu katika Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika.
Siku
hiyo, mabingwa wa zamani wa Afrika, TP Mazembe ya DRC watakuwa wenyeji wa
Medeama ya Ghana katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
Mechi
za Kundi B siku hiyo; Kawkab Marakech watakuwa wenyeji wa mabingwa watetezi
Etoile du Sahel katika mchezo wa Kundi B nchini Morocco, wakati F.U.S Rabat
watakuwa wenyeji wa Ahly Tripoli nchini Morocco pia.
Ikitoka
Algeria, Yanga itarejea nyumbani kuikaribisha TP Mazembe Juni 28, kabla ya
kumaliza na Medeama ya Ghana Julai 15, Dar es Salaam pia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni