KIONGOZI wa zamani wa Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema kwamba wanachama wengi wa klabu hiyo wamemfuata kumuomba agombee katika uchaguzi wa Juni, lakini anasikitika hataweza kutekeleza ombi lao.
“Watu wananitumia sms, wananipigia simu na wengine wamenifuata ofisini kwangu kuniomba nigombee. Tena wengine wanasema wanataka waniletee fomu nyumbani, au ofisini,
”amesema Bin Kleb akizungumza Kleb amesema aliamua kujitoa kwenye uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti, Yussuf Manji kutokana na kubanwa na shughuli zake binafasi mwaka jana na kwamba hadi sasa hakuna kilichobadilika.
Abdallah Bin Kleb (kushoto) akiwa na kiungo Haruna Niyonzima (kulia) |
“Nilimuomba Mwenyekiti (Manji) aniondoe kwenye uongozi baada ya kubanwa na shughuli binafasi ikiwemo masuala ya familia. Na hadi sasa hakuna mabadiliko, kwa sababu zile zile, sitagombea,”amesema Bin Kleb.
Hata hivyo, Bin Kleb amesema kwamba pamoja na kujitoa kwenye uongozi wa klabu, lakini ameendelea kushirikiana na uongozi uliopo madarakani na kutoa michango yake pia ya hali na mali.
“Ninashirikiana nao vizuri na wao wanajua. Hata baadhi ya wanachama walio karibu sana na timu wanajua kwamba bado ninasaidia Yanga. Vivyo hivyo, hata kwa uongozi ujao, nitaendelea kusaidia Yanga nikiwa nje ya uongozi,”amesema Bin Kleb.
Bin Kleb amesema kwamba anawashukuru wanachama wa Yanga kwa kuendelea kumuamini na kwa heshima wanayompa, lakini anawaomba radhi kwamba hataweza kwa sasa.
“Ila wasiwe na wasiwasi, mimi siyo Yanga wa kuchovya, mimi ni Yanga kindakindaki, au tuseme Yanga wa kulia, Yanga damu. Nitaendelea kuisaidia Yanga daima,”amesema.
Uchaguzi wa Yanga unatarajiwa kufanyika Juni 11 mwaka huu na leo wanachama wanatarajiwa kuanza kuchukua fomu makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam.
PICHA MANJI AKICHUKUA FOMU ZA KUGOMBEA UWENYEKITI YANGA;
Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji akilipia fomu za kugombea Uenyekiti wa Yanga leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni