KATIKA kile kilichoonekana kuwa wanachama wa klabu ya Simba wamepania kufanya mabadiliko katika mfumo wa uendeshaji, leo wamesikika wakifanya mabadiliko ya kauli mbiu yao ya 'Simba Nguvu Moja' na kuwa 'Simba Mabadiliko'.
Hayo yametokea asubuhi hii kwenye mkutano mkuu baada ya Rais wa klabu hiyo Evance Aveva kusimama ili kufungua mkutano huo ndipo aliposema 'Simba' akitarajia kujibiwa 'Nguvu Moja' katika hali ya kushangaza wanachama hao walijibu kwa pamoja 'Mabadiliko'.
Kabla ya hapo wanachama hao walilipuka kwa furaha pale iliposomwa ajenda ya tisa inayozungumzia maboresho ya mfumo wa uendeshaji huku ikionyesha wazi wanahitaji mabadiliko ya kuondoka kwenye mfumo wa Uanachama na kwenda kwenye Hisa.
Tayari mfanyabiashara Mohamed Dewji 'Mo' ameshaweka wazi nia yake ya kutaka kuwekeza katika klabu hiyo kwa kutoa kiasi Sh 20 Bilioni.
WAKATI HUO;
Aveva aliyasema hayo leo kwenye mkutano mkuu alipokuwa akiwasilisha taarifa kutoka Kamati ya Utendaji juu ya uendeshaji wa klabu hiyo kwa msimu wa 2015/16.
Rais huyo aliuambia mkutano mkuu kuwa wachezaji wengi wa kigeni waliosajiliwa msimu uliopita walikuwa wa viwango vya chini na hawakustahili kuichezea Simba.
"Tunakiri kuboronga katika usajili wa wachezaji wa kigeni, ni wazi usajili haukuwa makini na kwamba tulizitumia vibaya nafasi saba tulizopewa," alisema Aveva.
Katika hatua nyingine Aveva alisema matokeo mabaya ya Simba msimu uliopita yalitokana pia na kuwepo kwa wachezaji wasaliti katika kikosi hicho akitolea mfano wachezaji waliogoma kwenda Songea kwa madai ya kutolipwa mishahara yao.
"Tuligundua katika jeshi letu la msimu uliopita kulikuwa na wanajeshi wenye wasaliti, mshahara wa Simba unalipwa tarehe nane ilikuaje wachezaji wagome tarehe nane hiyo hiyo?," alihoji Aveva.
PIA kile kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu na wanachama wa Simba kimetimia baada ya mkutano mkuu kuridhia mabadiliko ya katiba ili kuingia katika mfumo wa Hisa.
Wajumbe wa mkutano huo ambao ulikuwa na ajenda 10 walionyesha tangu mwanzo kutaka mabadiliko huku wakiisubiri kwa hamu ajenda ya tisa ambayo ndiyo imekamilika kwa wanachama kupitisha mapendekezo hayo kwa kauli moja.
Baada ya ajenda hiyo Rais Evance Aveva alifunga mkutano huo na kuwaacha wanachama wakishangilia kwa nguvu.
Kutokana na ridhaa hii ya wanachama, Simba italazimika kuandaa mchakato wa jinsi gani sahihi ya kuingia katika mfumo wa Hisa huku Mfanyabiashara Mohamed Dewji 'Mo' akipewa nafasi kubwa zaidi ya kuwa mwekezaji mkuu.
NA BOIPLUS
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni