KUELEKEA
mchezo wa leo Jumatano wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga dhidi ya Azam, kuna mambo
mawili lazima yatokee ambayo kwa kila upande yatakuwa na maana kubwa sana.
Mchezo
huo ambao ni wa nne mfululizo kwa timu hizo kupambana katika Ngao ya Jamii, utapigwa
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ikumbukwe
kuwa, mchezo wa Ngao ya Jamii huwakutanisha mabingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe
la FA, lakini kutokana na Yanga kufanikiwa kuchukua makombe yote hayo, sheria
za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinaelekeza mshindi wa pili wa Kombe la FA
ndiye atakayecheza na bingwa wa ligi, ndiyo maana Azam wakapata nafasi hiyo.
Lakini
hata kama mshindi wa pili wa ligi ndiye angecheza na bingwa wa ligi, basi Azam
ingekuwa tena na nafasi hiyo kwani msimu uliopita imemaliza ikiwa nafasi ya
pili nyuma ya Yanga.
Katika
rekodi za Ngao ya Jamii, Yanga imefanikiwa kuibuka na ushindi mara tano katika
michezo saba iliyocheza. Mwaka 2001, iliifunga Simba mabao 2-1, mwaka 2009
ikafunga bao 1-0 dhidi ya Mtibwa.
Mwaka
2010, Yanga iliifunga Simba kwa penalti 3-1, baada ya mchezo kumalizika kwa
suluhu katika muda wa kawaida, lakini mwaka uliofuatia ikafungwa na Simba 2-0.
Baada
ya hapo, ikacheza tena mwaka 2013 dhidi ya Azam na kuibuka na ushindi wa bao
1-0, mwaka uliofuatia ikaifunga tena Azam mabao 3-0, kabla ya mwaka jana
kushinda kwa penalti 8-7 kutokana na muda wa kawaida kumalizika kwa suluhu.
Mara
ya kwanza kwa Yanga na Azam kukutana kwenye Ngao ya Jamii ilikuwa ni mwaka 2013
katika mchezo huo wa ufunguzi wa msimu wa 2013/14.
Kuanzia
hapo mpaka tunaelekea kuushuhudia mchezo wa leo, Azam haijawahi kuifunga Yanga
kwenye mechi tatu mfululizo za Ngao ya Jamii mfululizo timu hizo zilipokutana.
Kutokana
na hilo, leo Azam watataka kuiondoa rekodi hiyo mbaya kwao huku Yanga wakitaka
kuendeleza ubabe wao kwa Azam kwa lengo la kulinda heshima yao.
Rekodi ya Azam katika Ngao ya Jamii
Mara
ya kwanza kwa Azam katika historia yake kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii tangu
ilipopata nafasi ya kushiriki Ligi Kuu Bara mwaka 2007, ilikuwa ni dhidi ya Simba,
hiyo ilikuwa ni mwaka 2012 ambapo ilikubali kichapo cha mabao 3-2.
Miaka
mingine mbele baada ya kucheza na Simba, ikapambana na Yanga na mara zote
ikapoteza, hivyo mchezo wa leo kwa timu hiyo utakuwa na maana kubwa endapo itaibuka
na ushindi.
Matarajio ya wengi katika mchezo huu
Baada
ya Azam kulifanyia marekebisho makubwa benchi lake la ufundi kwa kumuondoa
Muingereza, Stewart Hall aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, ikamleta
Mhispania, Zeben Hernandez ambaye amekuja na wasaidizi wake kutoka nchini kwao.
Mpaka
sasa, kocha huyo amekiongoza kikosi cha Azam kucheza mechi nane za kirafiki,
imeshinda sita, sare mbili huku kikiwa hakijapoteza hata mchezo huo.
Kwa
maana hiyo, tunaweza kusema Yanga itakumbana na ushindani wa hali ya juu kwani
licha ya kocha huyo kuwa na kikosi hicho kwa muda mfupi, lakini tayari ameanza
kuonyesha makali yake.
Kwa
upande wa Yanga ambayo yenyewe haijapumzika tangu ilipomalizika ligi Mei, mwaka
huu kutokana na kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, tunaweza
kusema mechi hizo ilikuwa ikizitumia kujiweka fiti zaidi, hivyo wapo vizuri.
Usajili
iliyoufanya kwa kuwaongeza nyota kadhaa kikosini kwao, inakifanya kikosi hicho
kuwa kipana zaidi, kilichofanywa ni kusubiri mwisho wa mchezo matokeo
yatakuaje.
mdosejr@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni