KATIKA hali inayoonekana bundi mweusi kuanza kunyemelea katika klabu ya Yanga, mjumbe wa kamati ya utendaji wa klabu hiyo Salum Mkemi amefunguka kuwa mkutano mkuu uliopangwa kufanyika Jumamosi ijayo ni batili.
Mkemi alisema kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo mkutano mkuu wa wanachama unatakiwa kutangazwa siku 15 kabla huku agenda zikiwa zinafahamika lakini hadi kuelekea Jumamosi hakuna mtu anayejua wanaenda kujadili nini huku ukiwa umetangazwa kwa siku saba pekee.
Akizungumza Mkemi alisema mkutano huo ni batili kwakua umekiuka katiba ya Yanga ambapo hata wao Wajumbe wa kamati ya Utendaji hawajapewa barua juu ya hilo na hawajui hata ajenda zitakazojadiliwa.
"Kwa mujibu wa katiba yetu, mwenyekiti anapaswa kushauriana na kamati ya utendaji kuitisha mkutano mkuu wa dharura lakini katika hili hakuna mwanachama mwingine yoyote aliyeshirikishwa sasa huu sio utaratibu hauwezi kuongoza taasisi kwa matakwa yako binafsi," alisema Mkemi.
Akijibu tuhuma hizo Makamu Mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga alisema endapo mwanachama yoyote ana duku duku anapaswa kwenda kuzungumza katika mkutano mkuu na kufuata utaratibu wa kuongea na viongozi sio kulalamika kwenye vyombo vya habari.
"Hata hao wajumbe ni viongozi kama sisi, tulichaguliwa siku moja na wanachama kwahiyo kama wanaona kuna mapungufu sehemu wanatakiwa kufuata utaratibu na sio kulalamika ilibidi aje kwenye mkutano huo azungumze," alisema Sanga.
Jumamosi Agosti 6 Yanga watafanya mkutano mkuu wa dharura katika ukumbi Diamond Jubilee huku ajenda zitakazojadiliwa zikiwa hazijewekwa hadharani.
Boiplus
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni