Mabingwa watetezi Yanga ndio watakuwa wenyeji wa mpambano huo ambao umeteka hisia za wadau wengi wa soka nchini lakini wataingia uwanjani wakiwa tayari wamejeruhiwa kwa kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Stand United.
Simba wao ndio vinara wa ligi hiyo na hawaja poteza hata mchezo mmoja na pambano la Oktoba mosi, watapenda kuendeleza rekodi yao hiyo nzuri waliyoanza nayo msimu huu na kulipa kisasi cha kufungwa mechi zote mbili msimu uliopita.
Ukali wa pambano hilo hauna tofauti na ule wa La Liga kule nchini Hispania kati ya Real Madrid na FC Barcelona au pale England baina ya Manchester United na Manchester City na kule Italia unaweza kusema ni AC Milan na Inter Milan ingawa siku hizi hazina nguvu na Juve imekuwa ikitawala.
Ukilinganisha na miaka ya nyuma clasico ya msimu huu inatarajiwa kuongeza ushindani kutokana na matokeo ya msimu uliopita ambapo Simba walipoteza mechi zote mbili na kuwafanya wamalize msimu kwenye nafasi ya tatu matokeo ambayo yaliwaandama katika misimu mitatu iliyopita lakini msimu huu wameanza vizuri na ndio wanaoongoza ligi kwa sasa.
Kasi waliyoanza nayo Simba imewafanya kukusanya pointi 16 katika michezo sita waliyocheza hadi sasa ambapo wameshinda michezo mitano na kwenda sare mchezo mmoja huku wenyeji wao wa Jumamosi Yanga wakiwa wamecheza michezo mitano wameshinda mitatu sare mmoja na kufungwa mmoja wakiwa napointi 10 katika nafasi ya tatu.
Wakati mashabiki wa Simba wakionekana kuwa na uhakika wa pointi tatu mbele ya watani zao Yanga wao kidogo wameonyesha kuwa na hofu ya kupoteza pambano hilo kutokana na kiwango cha chini kilichoonyeshwa na timu yao katika mchezo uliopita dhidi ya Stand United ambao walipoteza kwa bao 1-0.
Pambano la Jumamosi ni wazi litakuwa ni la visasi kwani Simba hawatakuwa tayari kuona wanafungwa tena na mahasimu wao Yanga baada ya kupoteza mechi zote mbili msimu uliopita, lakini kocha Joseph Omog atataka kuendelea na rekodi yake nzuri aliyoanza nayo ya kubeba pointi tatu kuelekea kwenye kutimiza ahadi ya ubingwa.
Omog hiyo itakuwa ni mara yake ya kwanza kukutana na Yanga ambao ni mabingwa watetezi na walikuwa wawakilishi pekee kwenye michuano ya kombe la Shirikisho na kutolewa hatua ya makundi ni wazi anawajua wababe hao wa msimu uliopita na atahakikisha anakipanga vizuri kikosi chake ili na yeye aongeze akaunti yake ya pointi kupitia kwao.
Kocha Hans Pluijm siyo mgeni sana na Simba na tangu alipoanza kuifundisha Yanga ameshakutana na Simba mara tano na ameweza kushinda mechi tanu sare moja na kupoteza mchezo mmoja hivyo amekuwa na rekodi nzuri lakini pia mbali ya kuwa na rekodi hizo nzuri anajiavunia ubora wa kikosi chake ambacho kina wachezaji waliokaa pamoja kwa muda mrefu tofauti na Simba.
Simba ya msimu huu inautofauti mkubwa na ile ya msimu huu ujio wa wachezaji wpya kama Laudit Mavugo, Shiza Kichuya, Fredrick Blagnon , Muzamiru Yasini, Mussa Ndusha, Mohamed Ibrahim, Malika Ndeule na Jamvier Bukungu unaweza kuisaidia timu hiyo kurudishe furaha yake kutoka kwa watani zao Yanga ambao wenyewe wamesajili wachezaji watano wapya msimu huu ambao ni Obrey Chirwa, Hassan Ramadhan ‘Kessy’ Endrew Vicent, Juma Mahadhi na kipa Beno Kakolanya.
Lakini pamoja ya hayo yote ni vigumu kutabiri mshindi pindi timu hiz mbili zinapokutana kwani mara nyingi timu ambayo kwa kipindi hicho inaonekana dhaifu ndiyo inayoibuka na ushindi na kuwashangaza wengi na hapo upande wa pili unabakiwa na maumivu makubwa ambayo hupelekea hata kupoteza mwelekeo kwenye mechi zinazofuata.
Zifuatazo hapo chini ni rekodi mbali mbali za mapambano ya El clasico ya Tanzania Simba na Yanga ili uweze kujionea namna ambayo ushindani unavyokuwepo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita hadi mchezo wa Jumamosi Oktoba 1, 2016.
OKTOBA 16, 2010:
Yanga ilicheza na Simba kwenye uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza mchezo wa ligi ya Vodacom na Yanga kushinda bao 1-0 mfungaji akiwa Jeryson Tegete bao la dakika ya 70.
MACHI 5, 2011
Katika mchezo wa marudiano uliopigwa uwanja wa taifa Dar es Salaam timu hizo zilikutana na matokeo kuwa sare ya 1-1 Yanga walianza kufunga kupitia kwa Stephano Mwasika dakika ya 59 kwa njia ya penalti na Simba ilisawazisha dakika ya 73 kupitia kwa Musa Hassan ‘Mgosi’.
OKTOBA 29, 2011
Yanga iliendeleza ubabe kwenye ligi ya msimu uliofuata kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 Simba, Mzambia Davis Mwape ndiye mfungaji wa bao hilo pekee lililofungwa dakika ya 75 baada ya makosa ya beki wa Simba Victor Costa.
MEI 6, 2012
Simba ilifanya kufuru kubwa kwenye mchezo wa marudiano uliofanyika Mei 6 siku ya mwisho ya msimu huo baada ya kuifunga Yanga mabao 5-0.
Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 1 na 65, Patrick Mafisango pen dakika ya 58, Juma Kaseja pen dakika ya 69 na Felix Sunzu pen dakika ya 74.
OKT 3, 2012
Yanga wakiwa wenyeji wa mpambano huo walilazimishwa sare kwa kufungana bao 1-1 Simba
Mshambuliaji Amri Kiemba alianza kuifungia Simba mapema dakika ya tatu kabla ya Said Bahanuzi kuisawazishia Yanga kwa penalt dakika ya 64 baada ya beki Paol Ngalema kushika mpira akiwa ndani ya eneo la hatari.
OKTOBA 20,2013
Yanga ilishindwa kulipa kisasi cha mabao matano katika mchezo ambao hadi mapumziko walikuwa mbele kwa mabao 3-, lakini Simba walirudi kwa kasi kipindi cha pili na kusawazisha mabao yote na hadi dakika ya 90 matokeo yalikuwa 3-3.
Wafungaji wa Yanga katika mchezo huo walikuwa Mrisho Ngasa dk 14 na Hamisi Kiiza aliyefunga mabao mawili dakika za 35,47.
Wafungaji wa mabao ya Simba walikuwa ni Beatram Mwombeki dakika ya 53, Joseph Owino dakika ya 57na Gilbert Kaze dakika ya 83.
DESEMBA 21,2013 ‘Nani Mtani Jembe’
Mechi ya bonanza iliyoandaliwa na waliokuwa wadhamini wa timu hizo mbili na Yanga kufungwa mabao 3-1, na kupelekea kulitimua benchi lake lote la ufundi.
Mabao ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na
Amisi Tambwe aliyefunga mabao mawili na Awadhi Juma alifunga bao la mwisho dakika za majeruhi.
Huku Emmanuel Okwi akifunga bao pekee la Yanga ikiwa ndiyo mechi yake ya kwanza kuichezea timu hiyo baada ya kusajiliwa akitokea SC Villa ya kwao Uganda.
APRIL 20,2014
Timu hizo zilikutana kwenye mchezo wa ligi ya Vodacom na kutoka suluhu ya bila kwa kufungana mabao 1-1, Simba walianza kufunga kupitia kwa Haruna Chanongo na Yanga walisawazisha kupitia bao la dakika za mwisho la Simon Msuva.
OKTOBA 20, 2014
Timu hizo ziliendelea kuogopana baada ya kutoka sare ya bila kufungana huku Yanga ikiwa chini ya kocha Marcio Maximo na kipa wa Simba katika mchezo huo alikuwa Manyika Peter Chipukizi aliyekuwa anacheza mechi yake ya kwanza kubwa tangu aanze kucheza soka la ushindiani.
DESEMBA 21 2014 Nani Mtani Jembe
Simba iliendeleza ubabe wake kwa Yanga kwenye mechi za bonanza hilo kwa kuifunga Yanga mabao 2-0 matokeo ambayo tena yalimfukuzisha kocha Maximo na kusababisha kutua nchini Hans Pluijm kocha wa sasa wa Yanga.
Mabao ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na Awadhi Juma na Elisi Maguli alifunga bao la pili dakika ya 42 na mchezo huo kumalizika kwa Yanga kulala 2-0.
APRILI 18 2015
Simba iliendeleza wimbi la ushindi kwa ushindi wa bao 1-0, mbele ya Yanga katika mchezo wa ligi ya Vodacom huku bao hilo pekee likifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 51.
OKTOBA 20 2015
Msimu huu ulikuwa mgumu kwa Simba kwani licha ya timu yao kuwa na mapungufu makubwa lakini pia uongozi wa timu hiyo haukuwa na maelekewano mazuri na katika mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa taifa Simba wakalala kwa mabao 2-0.
Wafungaji wa Yanga walikuwa ni Amissi Tambwe na Malimi Busungu .
FEBRUARI 20,2016
Huu nimchezo wa marudiano wa ligi ya Vodacom ambao ulizikutanisha timu hizo mbili zenye uhasama mkubwa na Simba iliendelea kuambulia kipigo cha mabao 2-0, kama ilivyokuwa kwenye mzunguko wa kwanza.
Mabao ya Yanga kwenye mchezo huo uliopigwa uwanja wa taifa yalifungwa na Donald Ngoma aliyefunga bao la kwanza na Amissi Tambwe alimalizia bao la pili kipindi cha pili na huo ndio kuwa mchezo wa mwisho kuelekea pambano la Jumamosi.
Swali kubwa ambapo linaumiza vichwa vya mashabiki wa pande zote mbili ni Yanga kuendeleza ubaba wa msimu uliopita kwa Simba au Simba itakataa uteja huo kutokana na uimara wa kikosi chake cha msimu huu? tusubiri dakika 90 za mchezo huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni