BAADA ya kutokea uvumi kwenye mitandao ya kijamii, Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF limethibitisha mchezo kati ya Simba na Azam uliokuwa uchezwe Jumamosi ijayo umesogezwa mbele hadi Septemba 24.
Mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wengi wa soka nchini umesogezwa mbele kupisha mechi ya kufuzu michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 kati ya Serengeti boys dhidi ya Congo Brazzaville.
Ofisa Habari wa TFF Alfred Lucas amesema kuwa mchezo huo umesogezwa kwa wiki moja mbele ili kupisha mchezo huo wa timu ya vijana, na endapo wakishinda na kutoka walau sare kwenye mechi ya marudiano watakuwa wamefuzu moja moja katika michuano hiyo itakayofanyika mwakani nchini Madagascar.
"Mchezo kati ya Simba dhidi ya Azam umesogezwa mbele kwa wiki moja kupisha mechi ya vijana, mtanange huo utapigwa Septemba 24" alisema Lucas.
Kwa upande wa timu ya Simba kupitia kwa Msemaji wao Hajji Manara alisema kuwa wao hawawezi kuzungumza chochote kuhusu kusogezwa kwa mchezo huo mpaka watakapo pewa barua na TFF.
"Sisi klabu ya Simba hatujui chochote kuhusu hilo tunasubiri tupewe barua na TFF ndiyo tunaweza kuzungumza lakini kwa sasa hatuna cha kuongea" alisema Manara.
Msemaji wa Wana ramba ramba Azam FC Jaffar Iddi Maganga alisema hata wao wanasikia kwenye mitandao na hawana taarifa rasmi toka TFF wakizipata ndo watajua wafanyaje.
"Ndo tumerudi jana toka jijini Mbeya na leo ni sikukuu kwahiyo tunasubiri barua toka TFF ili tujue tunatoa msimamo gani" alisema Maganga.
STORI YA PILI;
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amemzawadia gari aina ya Toyota Raum beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kutokana na kazi yake nzuri kwa sasa katika klabu.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amemzawadia gari hilo Tshabalala asubuhi ya leo ofisini kwake, Mbezi Tangi Bovu, Dar es Salaam.
Na Hans Poppe akasema anaweza kutoa zawadi ya aina hiyo kwa mchezaji yeyote mwingine wa Simba SC atakayefuata nyayo za Tshabalala kwa kujituma na kuisaidia timu.
Hans Poppe (kulia) akimkabidhi kadi ya gari Tshabalala leo Dar es Salaam
Poppe amesema zawadi hiyo iliyoambatana na fedha taslimu Sh. Milioni 1 ya mafuta kwa miezi sita, haimo kwenye vipengele vya Mkataba wake wa sasa unaomalizika mwishoni mwa msimu.
“Hiyo ipo nje ya Mkataba wake, nimempa zawadi tu kutokana na juhudi zake kwa sasa. Na nitatoa zawadi hiyo kwa yeyote ambaye atafuata nyayo zake. Na nadhani zawadi kama hii inanukia kwa Ibrahim Hajib,”amesema Poppe.
Tshabalala aliye katika msimu wake wa pili Simba SC tangu asajiliwe kutoka Kagera Sugar amekuwa mchezaji muhimu kwenye timu hiyo kwa sasa.
Pamoja na kufanya vizuri kazi yake ya ulini, lakini pia Tshabala amekuwa akihusika karibu katika kila bao la Simba, aidha kwa kutoa pasi ya moja kwa moja au kusaidia shambulizi la bao.
..............
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni