Pambano la Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga limemalizika kwa Simba kuwabadilikia watani wao kwa kutoka nyuma na kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 2-1 leo jioni.
Kama ilivyo kuwa katika mchezo wa kwanza baina yao msimu huu alikuwa ni Shiza Kichuya aliyemaliza ubishi na kuwakata maini mashabiki wa Yanga kwa bao tamu la ushindi.
Yanga walianza mchezo wa vizuri a kufanikiwa kupata bao la mapema dakika ya 5 tu kufuatia beki wa Simba, Novalty Lufunga kumuangusha Obrey Chirwa ndani ya sanduku la hatari na mwamuzi Mathew Akrama kuamuru mkwaju wa penati.
Simon Msuva alipiga penati kiufundi kwa kuuficha mpira eneo la pembeni kabisa mbali na mikono ya kipa wa Simba Daniel Agyei.
Simba walifanya mabadiliko ya mapema ya kumtoa Juma Liuzio aliyeonekana kumezwa katika safu ya ulinzi ya Yanga na kumpa nafasi Said Ndemla aliyeongeza uhai katika kiungo cha Yanga.
Simba iliandamwa na balaa katika kipindi cha pili baaada ya beki wake mzoefu, Janvier Bokungu kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kumfanyia madhambi Obrey Chirwa.
Iliwabidi Simba kumtoa Mo Ibrahim na kumuingiza Jonas Mkude kujaribu kuweka sawa mambo. Mabadiliko mengine ya Simba ikiwemo lile la kumtoa Lufunga na kumuingiza Shiza Kichuya yalizaa matunda ya faraja.
Dakika ya 66 Laudit Mavugo aliisawazishia Simba kwa bao la kichwa.
Dakika ya 80 Kichuya akafunga bao la muhimu zaidi kwa kupiga ndizi hatari iliyomshinda kipa wa Yanga, Deogratius Munishi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni