TIMU ya Yanga imetolewa kwenye michuano ya kombe la klabu bingwa barani Afrika baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Zanaco FC ya Zambia kwenye uwanja wa Mashujaa nchini humo lakini hiyo ni kama ufunguo wa mlango mwingine wa kwenda kucheza michuano ya shirikisho.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam Jumamosi iliyopita timu hizo zilitoka sare ya bao moja hivyo Zanaco kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kushushwa hadi kwenye kombe la Shirikisho kutokana na kutolewa kwenye michuano ya klabu bingwa ambapo watakwenda kucheza mechi za mtoano na wakivuka watatinga hatua ya makundi.
Kwenye mchezo huo Yanga ilicheza kwa kasi ambapo dakika ya 20 mshambuliaji Obrey Chirwa alikosa nafasi ya kufunga akiwa anatazama na nyavu baada kushindwa kumalizia mpira uliopigwa na Thaban Kamusoko.
Wenyeji nao mara kadhaa walijibu mapigo kwa kushambulia lango la Yanga lakini safu ya ulinzi iliyokuwa chini ya Kelvin Yondani na Vincent Bossou ilikuwa imara kumlinda golikipa Deogratius Munishi ‘Dida’.
Beki wa kulia wa Yanga Hassan Kessy alicheza vizuri upande huo kama alivyofanya katika mchezo wa kwanza kwa kukaba na kupiga krosi lakini changamoto ilikuwa ni kwenye umaliziaji.
Kikosi cha Yanga leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Justin Zulu, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Obrey Chirwa na Geoffrey Mwashiuya/Emmanuel Martin dk62.
Zanaco; Toster Sambata, Ziyo Tembo, George Kilufya, Zimeselema Moyo/, Chongo Chirwa, Saith Sakala, Taonga Bwembya, Ernest Mbewe, Boyd Musonda, Attram Kwame na Augustine Mulenga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni