NYOTA wapya waliosajiliwa na timu vigogo hapa nchini za Simba na Yanga watakutana katika mchezo wa kwanza baina ya miamba hiyo katika mechi ya ngao ya hisani itakayofanyika Agosti 23 uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kumaliza ubishi wa nani katisha kwenye usajili.
Kivutio kikubwa kwenye mchezo huo kitakuwa mshambuliaji Ibrahim Ajib ambaye amekulia katika klabu ya Simba na kujiunga na Yanga msimu huu na Emmanuel Okwi ambaye amerejea Simba kwa mara ya tatu huku ikionekana matumaini ya Wekundu hao yapo kwake.
Tayari Ajib ameanza kuonekana na mabingwa hao katika mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya huku Okwi akiwa bado hajarudi kujiunga na wenzake tangu aliposaini mkataba wa Wekundu hao mwezi uliopita.
Nyota wengine ambao watacheza mechi hiyo kwa mara ya kwanza ni mlinda mlango Youthe Rostand na beki Abdallah Haji ‘Ninja’ kwa upande wa Yanga huku John Bocco, Yusuph Mlipili, Shomari Kapombe, Ally Shomari, Jamal Mwambeleko na Emmanuel Mseja wakitarajiwa kutetea jahazi la Simba.
Mechi hiyo inaashiria ufunguzi wa ligi kuu ya Vodacom kwa msimu wa 2017/18 ambayo itaanza Agosti 26 huku miamba hiyo ikikutana Oktoba 14 katika mchezo wa kwanza wa ligi Simba ikiwa mwenyeji.
Katika siku ya kwanza Agosti 26 kutachezwa mechi saba katika viwanja mbalimbali huku mchezo mmoja kati ya mabingwa watetezi Yanga dhidi ya Lipuli utapigwa siku moja baadae.
Michezo hiyo imepangwa kama ifuatavyo:
Ndanda vs Azam FC Mwadui FC vs Singida United Mtibwa Sugar vs Stand United Simba vs Ruvu Shooting Kagera vs Mbao FC Njombe Mji vs Prisons Mbeya City vs Majimaji
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni