Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF limefanya ukaguzi wa Viwanja vitakavyotumika kwenye raundi ya 4 ya Kombe la Shirikisho la Azam ASFC.
Baada ya ukaguzi huo sasa JKT Tanzania watatumia Uwanja wa Azam Complex kwa mchezo wake dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara wakati Kiluvya United watatumia Uwanja wa Mabatini Mlandizi kwa mchezo wake dhidi ya Tanzania Prisons.
Michezo hiyo imehamishwa kwasababu ya viwanja hivyo kutokidhi viwango vya kikanuni baada ya wataalamu kutoka idara ya Ufundi TFF kufanya ukaguzi.
Ifahamike kuwa kanuni ya 7(7) ya ASFC inatamka kuwa TFF ina mamlaka ya mwisho kuhamisha mchezo husika katika Uwanja mwingine au kubadilisha kituo cha mchezo kwasababu inazoona zinafaa kwa mchezo na wakati husika.
Ratiba inaonesha kuwa Februari 21 kutakuwa na mchezo utakaowakutanisha Njombe Mji vs Mbao FC utakaochezwa Uwanja wa Sabasaba Njombe,Februari 24 Singida United watakuwa Uwanja wa Namfua Singida kucheza dhidi ya Polisi Tanzania saa 10 jioni wakati KMC watacheza dhidi ya Azam FC saa 1 usiku Azam Complex,Chamazi.
Mechi nyingine zitachezwa Februari 25 wakati Buseresere watakapowakaribisha Mtibwa Sugar saa 8 mchana kwenye Uwanja wa Nyamgana nao Majimaji FC ya Songea watakuwa Uwanja wa Majimaji kuwakaribisha Young Africans saa 10 jioni na saa 1 usiku Azam Complex JKT Tanzania watawakaribisha Ndanda FC kutoka Mtwara.
Februari 26 Kiluvya United watawakaribisha Tanzania Prisons kutoka Mbeya uwanja wa Mabatini saa 8 mchana na Kambarage pale Shinyanga Stand United watacheza na Dodoma FC saa 10 jioni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni