Gwiji wa soka kutoka nchini Ufaransa Zinedine Yazid Zidane, ametangaza kujiuzulu nafasi ya umeneja wa kikosi cha mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid, ikiwa ni siku kadhaa baada ya kuiwezesha klabu hiyo kuweka historia barani humo kwa kuifunga Liverpool, kwenye mchezo wa fainali uliopigwa mjini Kiev, Ukraine.
Zidane ametangaza maamuzi ya kujizulu nafasi yake leo mchana, na kuwashangaza wadau wengi wa soka duniani, ambao waliamini huenda angeendelea na majukumu yake huko Santiago Bernabeu, hasa baada ya kupata mafanikio ya kutwaa mfululizo mataji matatu ya Ulaya.
Gwiji huyo ambeya aliitumikia Real Madrid kama mchezaji kuanzia mwaka 2001–2006, ametangaza maamuzi ya kujiuzulu akiwa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Madrid, Hispania.
Amesema maamuzi alioyachukua hayajashurutishwa na hatua yoyote kutoka kwa viongozi wa juu, bali amefanya hivyo kwa kutaka mwenyewe, huku akiamini wakati wake wa kutoa huduma klabuni hapo umefikia kikomo, hivyo hana budi kuwapisha wengine
Amesema anaamini mashabiki wengi watakua wameshutushwa na maamuzi hayo, lakini amewaomba kuyaheshimu, huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Real Madrid endapo atahitajika.
“Nimeamua kuchukua maamuzi haya, kwa kuona sina nafasi ya kuendelea zaidi, ninaamini hapa nilipofika panatosha,” amesema Zidane.
” Maamuzi haya ni sahihi kwangu na kwa upande wa uongozi wa Real Madrid, sikutarajia kama ningefanya hivi hii leo, lakini nimekaa na kutafakari, nimebaini kuna haja wa kuondoka na kumuachia kazi mtu mwingine ambaye atakuja baada yangu.
“Nimefanya kazi vizuri na kila mmoja klabuni hapa, mafanikio nilioyapata hayakua juhudi zangu pekee yangu, yalikuja baada ya kuwa na ushirikiano katika kila hatua niliyokua nikipitia,”
“ Ninawashukuru sana wachezjai wangu wote niliobahatika kufanya nao kazi, ninaushukuru uongozi wa Real Madrid, pia sitawaacha mashabiki ambao walituonyesha ushirikiano katika michezo ya nyumbani na ugenini kila tulipokwenda.” Amesema Zidane.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni