BAADA ya fedheha kubwa ya kulikosa Kombe la Dunia kwa mara ya Pili kwenye Fainali za Nyumbani kwao, tena safari hii wakibondwa Bao 7-1 na Mabingwa wapya Germany kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Dunia, Brazil sasa wameanza kujiganga wenyewe.
Jana Brazil ilianza kuisimamisha Kamisheni ya Ufundi mpya kwa kumteua Mratibu wake ambae ni Gilmar Rinaldi aliewahi kuwa Kipa wao wa Akiba walipotwaa Kombe la Dunia Mwaka 1994.
Uteuzi huu unafuatia kuondoka madarakani kwa Kocha wa Brazil Luiz Felipe Scolari na Wasaidizi wake wote na pia hatua ya CBF, Shirikisho la Soka la Brazil, kuwafukuza Daktari wa Timu na Mkuu wa Habari.
Rais wa CBF, Jose Maria Marin, ambae Mwakani Mwezi Aprili anakabidhi madaraka kwa
Marco Polo Del Nero, amesema Wiki ijayo watateua Kocha mpya wa Brazil
Mratibu mpya wa Kamisheni ya Ufundi, Gilmar, mwenye Miaka 55, amenena: “Sasa inabidi tusikilize Watu. Hatuna haja kumuiga Mtu. Kitu muhimu ni kuchagua nini tunataka na kuweka misingi imara kwa ajili ya baadae.”
Gilmar aligusia tabia iliyozuka wakati wa Kombe la Dunia pale Neymar alipoumia kwa Washabiki kutoa ujumbe ‘Forca Neymar’ [Yaani: Nenda Neymar!] wakati ujumbe sahihi ulitakiwa kuhimiza Wachezaji waliokuwepo na wangesema ‘Forca Bernard!’
Huko Brazil zipo dalili kuwa Kocha wa zamani wa Klabu ya Corinthians, Tite, ndie atakuwa mrithi wa Scolari.
Tite, Jina kamili Adenor Leonardo Bacchi, alitwaa Copa Libertadores na pia Kombe la FIFA la Klabu Bingwa Duniani, baada ya kuifunga Chelsea, Mwaka 2012
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni