Kocha mkuu wa Simba sc Patrick Phiri akiongea na wachezaji wake
RATIBA ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa
2014/2015 utakaoanza kutimua vumbi septemba 20 mwaka huu imeanikwa hadharani na
Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF.
Afisa habari na mawasiliano wa TFF, Boniface
Wambura Mgoyo katika taarifa yake amesema ratiba hiyo imezingatia michuano ya
Chalenji itakayochezwa Novemba, usajili wa dirisha dogo Nov 15- Des 15,
ushiriki wa klabu za Azam na Yanga kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa (CL)
na Kombe la Shirikisho (CC).
Wambura alisema mechi zitachezwa wikiendi ili
kuongeza msisimko/kuwapa fursa washabiki wengi zaidi kuhudhuria, na katikati ya
wiki imeachwa wazi kwa ajili ya mechi za Kombe la FA (Federation Cup).
Vilevile kutakuwa na mechi Boxing Day na siku ya
Mwaka Mpya.
Siku ya ufunguzi zitapigwa mechi saba katika
viwanja tofauti nchini ambapo mabingwa watetezi Azam fc wataanza kutetea ubingwa wao dhidi ya
wageni Polisi Morogoro katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es
saalam.
Yanga chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo
wataanza ugenini katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro dhidi ya wakata miwa
wa Mtibwa Sugar.
Timu mbili zilizopanda ligi kuu msimu huu, Stand
United na Ndanda fc zitachuana katika dimba la Kambarage mkoani Shinyanga.
Mgambo JKT watakawakaribisha Kagera Sugar katika
dimba la CCM Mkwakwani jinni Tanga.
Ruvu Shooting wataanza kampeni zao katika uwanja
wao wa Mabatini uliopo Mlandizi Pwani dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons.
Wagonga nyumbo wa Mbeya City fc wataanza nyumbani
katika dimba la CCM Sokoine Mkoani Mbeya dhidi ya JKT Ruvu.
Kocha mkuu wa Yanga sc, Marcio Maximo (kushoto)
Wekundu wa Msimbazi Simba chini ya kocha Mzambia,
Patrick Phiri wao wataanza kampeni za kuusaka ubingwa wa ligi kuu bara septemba
21 dhidi ya Coastal Union uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Raundi ya pili
itacheza septemba 27 na 28 mwaka huu ambapo timu zote zitashuka dimbani.
Septemba 27, wekundu wa Msimbazi Simba watacheza
mechi yao ya pili nyumbani dhidi ya Polisi Morogoro.
Mechi nyingine siku hiyo zitakuwa baina ya Mtibwa
Sugar dhidi ya Ndanda fc katika uwanja wa Manungu Turiani. Azam watawakaribisha
Ruvu Shooting Chamazi, Mbeya City watachuana na Coastal Union uwanja wa
Sokoine, wakati Mgambo JKT watakuwa Mkwakwani kuchuana na Stand United.
Raundi ya pili itakamilika septemba 28 ambapo JKT
Ruvu watavaana na Kagera Sugar katika uwanja wa Azam Complex.
Mechi nyingine itawakutanisha Yanga sc ya Maximo
dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Endelea kufuatilia mtandao huu kwasababu
utaendelea kukujuza kuhusu ratiba nzima ya ligi kuu soka Tanzania bara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni