Kipa namba moja wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed 'Nduda', amewaambia Simba kuwa atakuwa tayari kusaini mkataba na klabu hiyo kama itatoa Sh milioni 50 na mshahara mnono wa Sh milioni 3 kwa mwezi, vinginevyo atakuwa tayari kwenda kucheza bure Majimaji.
Huo unaonekana kuwa mtihani mkubwa kwa Simba ambayo ipo katika harakati za kumsajili kipa bora huyo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyofanyika mwanzoni mwa mwaka huu Zanzibar.
Mohamed amesema kuwa kwa sasa hiyo ndiyo thamani yake kutokana na kuwa katika kiwango kizuri.
Alisema kama atajiweka sokoni kwa vijesenti vya mboga ambavyo havitakuwa na msaada wowote maishani mwake, atakuwa hajitendei haki, pia hajithamini mwenyewe .
“Bado naendelea na mazungumzo na viongozi wa Simba lakini mpaka sasa bado hatujafikia makubaliano kwani dau wanalotaka kunipatia ni dogo, halilingani na thamani yangu kwa sasa”. Mohamed amekaririwa na Salehjembe.
“Ukiangalia kazi niliyofanya msimu uliopita, kila mtu anayejua soka atakuwa anaijua thamani yangu, nimewaambia wanipatie milioni 50 na mshahara wa milioni tatu kwa mwezi, lakini wanaonekana kutokuwa tayari kutoa fedha hizo, hivyo kama watashindwa basi ni heri nikaendelea kubakia Mtibwa au nikarudi katika timu yangu ya zamani ya Majimaji ambayo pia inanihitaji,” alisema Mohamed.
Kipa huyo kwa sasa ni mchezaji huru, hana mkataba na timu yoyote ile kwani muda wake wa kuitumikia Mtibwa Sugar umefikia tamati hivi karibuni baada ya kumalizika kwa michuano ya Ligi Kuu Bara.
CHANZO : MPENJA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni