MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amefunga bao moja na kuseti moja, TP Mazembe ikitimiza dhamira ya kutwaa ubingwa wa Afrika baada ya kuifunga 2-0 USM Alger ya Algeria.
Mchezo huo wa marudiano wa fainali ya Ligi ya Mabingwa uliofanyika Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, wenyeji walipata mabao yote kipindi cha pili.
Na Mazembe inatwaa taji la tano la Ligi ya Mabingwa kwa ushindi wa jumla wa 4-1, baada ya awali kushinda 2-1 mjini Algiers Jumapili iliyopita.
Samatta akipongezwa na Mtanzania mwenzake, Thomas Ulimwengu baada ya kufunga |
Samatta leo aliwekewa ulinzi mkali na wachezaji wa USM hadi akalazimika kusubiri kufunga bao lake la saba katika michuano ya mwaka huu kwa penalti dakika ya 75, baada ya Rogger Asale kuangushwa.
Samatta
naye akamsetia pasi nzuri Assale kufunga bao la pili katika dakika za
majeruhi baada ya kutimia dakika 90 za kawaida za mchezo.
Matokeo
hayo yanamfanya Samatta pia awe mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa msimu
huu, baada ya kufikisha mabao saba.
Hii
maana yake huu unakuwa mwaka wa pili mfululizo, Tanzania inatoa
mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa, baada ya mwaka jana Mrisho Khalfan
Ngassa kuongoza pia akiwa na klabu ya Yanga SC, kabla ya kuhamia Free
State Stars ya Afrika Kusini msimu huu.
Ngassa
alifunga mabao sita sawa na El Hedi Belameiri wa Setif, Haythem Jouini
wa Esperance na Ndombe Mubele aliyekuwa AS Vita ya DRC, sasa Al Ahly.
Kikosi
cha TP Mazembe kilikuwa; Muteba Kidiaba, Joel Kimuaki Mpela, Salif
Coulibaly, Mbwana Samata, Adama Traore, Kissi Boateng, Solomon
Asante/Rogger Asalle dk46, Thomas Ulimwengu/Daniel Adjei Nii dk90, Mikis
Mina/Merveille Bokadi dk72, Boubacar Diarra na Yaw Frimpong.
USM
Alger; Mohamed Zemmamouche, Arslane Mazari/Farouk Chafai dk51, Hocine
El Orfi, Rachid Nadji, Houcine Benayada/Mohamed Amine Aoudia dk70,
Nacereddine Khoualed, Hamza Koudri, Mokhtar Benmoussa/Ayoub Abdellaoui
dk90, Brahim Boudebouda, Kaddour Beldjilali na Zinedine Ferhat.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni