YANGA SC imevunja Mkataba na kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kutokana na mchezaji huyo wa Amavubi kukiuka vipengele.
Katibu Mkuu wa Yanga SC, Dk Jonas Tiboroha amewaambia Waandishi wa Habari katika Mkutano uliofanyika makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam kwamba Haruna pia anatakiwa kuilipa klabu.
Tiboroha amesema uamuzi huo umefikiwa na kikao cha Kamati ya Nidhamu ya klabu, baada ya kulichunguza kwa umakini suala la mchezaji huyo na historia yake ya nidhamu pia ndani ya klabu tangu asajiliwe miaka minne iliyopita.
Sakata la sasa la Niyonzima linaanzia mwezi uliopita baada ya mchezaji huyo kuruhusiwa kwenda kuichezea Rwanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki, CECAFA Challenge nchini Ethiopia na akachelewa kurejea baada ya mashindano.
Kufuatia hali hiyo, klabu ilimsimamisha kwa muda usiojulikana Niyonzima kabla ya suala lake kupelekwa Kamati ya Nidhamu, ambayo hatimaye imekuja na maamuzi magumu.
Pamoja na Niyonzima kuwasilisha vielelezo vyote vya kumsafisha, lakini uchunguzi wa Kamati ya Nidhamu ulijiaminisha kiungo huyo amedanganya ili kukwepa hatua za kinidhamu.
Ulibaini plasta gumu (PoP) alilofunga baada ya kurejea akiwa amechelewa ilikuwa ni ‘geresha’ na vielelezo vingine alivyowasilisha vilikuwa ‘feki’ pia.
Na ikamnasa kwenye picha za video siku za karibuni ‘akijirusha’ sehemu mbalimbali za starehe ikiwemo kwenye onyesho la mwanamuziki Ali Kiba.
Haruna aliyezaliwa Februari 5, mwaka 1990 Gisenyi nchini Rwanda, alijiunga na Yanga SC mwaka 2011 akitokea APR ya kwao, ambako aliwasili mwaka 2007 akitokea Rayon aliyoichezea kwa misimu miwili baada ya kujiunga nayo akitokea Etincelles iliyomuibua mwaka 2005.
Haruna Niyonzima amefukuzwa Yanga SC kwa tuhuma za utovu wa nidhamu |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni