TIMU ya VfL Wolfsburg imeitupa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Manchester United baada ya kuichapa mabao 3-2 katika mchezo wa Kundi B Uwanja wa Volkswagen Arena usiku wa kuamkia leo.
Wolfsburg inamaliza na pointi 12, ikifuatiwa na PSV pointi 10, wakati United inabaki na pointi zake nane- hivyo inahamia kwenye michuano ya Europa League.
Mbaya wa United alikuwa ni Ronaldo Aparecido Rodrigues aliyefunga mabao mawili jana dakika ya 13 na 84, wakati bao lingine la wenyeji limefungwa na Adelino Andre Vieira de Freitas dakika ya 29.
Mabao ya United yamefungwa na Anthony Martial ambalo lilikuwa la kwanza mchezoni dakika ya 10, wakati lingine Wolfsburg walijifunga kupitia kwa Josuha Guilavogui dakika ya 82.
Kipa wa United, David De Gea akiwa hoi baada ya mchezaji mwenzake, kushindwa kumzuia Naldo kuifungia Wolfsburg bao la ushindi
Mchezo mwingine wa kundi hilo, PSV imeshinda 2-1 dhidi ya CSKA Moscow mabao yake yakifungwa na Luuk de Jong dakika ya 78 na Davy Propper dakika ya 85, huku la wageni likifungwa na Sergei Ignashevitch kwa penalti dakika ya 76 Uwanja wa Philips.
Real Madrid imefanya ‘unyama’ ikishinda 8-0 dhidi ya Malmo FF katika mchezo wa Kundi A, Cristiano Ronaldo peke yake akifunga manne, Karim Benzema mawili na moja Mateo Kovacic Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Mchezo mwingine wa kundi hilo, Paris Saint-Germain imeichapa 2-0 Shakhtar Donetsk mabao ya Lucas Rodrigues Moura da Silva dakika ya 57 na Zlatan Ibrahimovic dakika ya 86 Uwanja wa Parc des Princes.
Real inamaliza na pointi 16, ikifuatiwa na PSG 13, wakati Shakhtar iliyovuna pointi tatu tu nayo inakwenda Europa League.
Manchester City imeshinda 4-2 dhidi ya Borussia Monchengladbach katika mchezo wa Kundi D Uwanja wa Etihad, Raheem Sterling akifunga mabao mawili dakika ya 79 na 81, mengine David Silva dakika ya 16 na Wilfried Bony dakika ya 85, huku ya wageni yakifungwa na Julian Korb dakika ya 19 na Raffael Caetano de Araujo dakika ya 42.
Mchezo mwingine wa kundi hilo, Sevilla imeichapa bao 1-0 Juventus, mfungaji Fernando Llorente dakika ya 65 Uwanja wa Ramon-Sanchez Pizjuan.
Man City inamaliza na pointi 12, ikifuatiwa na Juve 11, wakati Sevilla yenye pointi sita inahamia Europa League.
Raheem Sterling akishangilia baada ya kuifungia mabao mawili Manchester City
Atletico Madrid imeshinda 2-1 ugenini dhidi ya Benfica katika mchezo wa Kundi C, mabao yake yakitiwa kimiani na Saul Niguez dakika ya 33 na Luciano Vietto dakika ya 55, kabla ya Kostas Mitroglou kuwafungia wenyeji la kufutia machozi dakika ya 75 Uwanja wa Luz.
Mchezo mwingine wa kundi hilo, Galatasaray imetoa sare ya 1-1 na FC Astana bao lake likifungwa na Selcuk Inan dakika ya 64 na wageni likifungwa na Patrick Twumasi dakika ya 62 Uwanja wa Turk Telekom Arena.
Atletico inamaliza na pointi 13, ikifuatiwa na Benfica pointi 10, wakati Galatasaray iliyomaliza na pointi tano, inahamia Europa League.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni