KUNA msemo unaosema duniani wawili wawili. Msemo huu
umeonekana kukubalika kwa jamii zote kutokana na jinsi mambo yanayotokea
duniani kila kukicha.
Achana kwa kufanana kwa
vitu ambavyo vinaweza kutengenezwa na binadamu, hapa msemo huu unagusa kile
kinachopangwa na Mungu.
Unaweza kukuta watu
wakifanana licha ya kutokuwa ndugu na mifano mingine mingi kama hiyo.
Katika
Ligi Kuu ya England ‘Premier’, kuna timu inaitwa Leicester City, mwanzoni mwa
msimu huu timu hii haikuwa ikitajwa sana wala kupewa nafasi ya kuja kutikisa
vigogo katika Premier, lakini kwa sasa imekuwa midomoni mwa watu wengi kutokana
na kile inachokifanya.
Timu za Arsenal,
Manchester United, Manchester City, Chelsea na hata Liverpool, ndizo zilikuwa
zikipewa nafasi kubwa sana ya kufanya vizuri mpaka kufikia siku ya Sikukuu ya
Krismasi.
Imekuwa kawaida kwa
timu hizo kujiwekea malengo hayo huku zikiamini hiyo ni njia mojawapo ya
kujitengenezea mazingira ya kutwaa ubingwa.
Leo ndiyo Krismasi, na ukiangalia
msimamo wa ligi hiyo, utaikuta Chelsea ipo nafasi ya 15, Liverpool ya tisa,
Machester United ya tano, Manchester City inakamata nafasi ya tatu huku Arsenal
ikiwa ya pili, kwenye ile nafasi ambayo timu hizo zimekuwa zikiilenga, wapo
vijana wa Muitaliano, Claudio Ranieri, Leicester City.
Leicester iliyoanzishwa
miaka 131 iliyopita, inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 38 ambazo ni mbili
zaidi ya Arsenal. Mbali na kuongoza ligi, pia straika wao tegemezi, Jamie Vardy
anaongoza kwa ufungaji akiwa amefunga mabao 15.
Vardy ambaye anaonekana
kuwa mwiba kati ya mastraika wa timu zote 20 za ligi hiyo, hivi karibuni
alivunja rekodi ya gwiji wa zamani wa, Manchester United, Ruud van Nistelrooy.
Rekodi hiyo ni ile ya kufunga mabao kwenye mechi 11 mfululizo.
Vardy yeye amefikisha mechi 12 akifunga
mfululizo. Leicester ama unaweza kuiita Jeshi la Bluu kama inavyojulikana kwa
jina lake la utani, inaendelea kupambana na vigogo lakini hali kama hiyo
inatukumbusha msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara.
Ligi Kuu Bara ambayo
msimu uliopita ilikuwa inazihusisha timu 14, Yanga ndiyo ilikuwa bingwa
ikifuatiwa na Azam, lakini tangu kuanza kwa ligi hiyo mpaka ilipofika Januari,
mwaka huu wakati ligi imesimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi, Mtibwa
Sugar ndiyo ilikuwa ikishikilia usukani.
Kila mmoja alianza kuwaza safari ya ubingwa
kwa Mtibwa inaelekea vizuri baada ya kufanya hivyo miaka miwili mfululizo, 1999
na 2000.
Lakini ligi ilipoendelea baada ya Kombe la Mapinduzi kumalizika, kibao
kikageuka, Mtibwa ikajikuta inaanza harakati za kujikwamua kushuka daraja, kwa
bahati nzuri haikushuka, ilimaliza msimu ikiwa nafasi ya saba.
Kinachozifelisha timu
nyingi duniani kote, ni kutokana na wachezaji wao tegemezi kupata majeraha ya
muda mrefu. Hicho ndicho kilichovuruga mipango ya vijana wa beki wa zamani wa
Taifa Stars, Mecky Maxime, timu ya Mtibwa Sugar.
Katika wachezaji
tegemezi wa Leicester, huwezi kuacha kumtaja Riyad Mahrez na Vardy ambao
wamekuwa wakicheza kila mechi, na endapo mmoja wao ama wote wawili wakija
kupata majeraha yatakayowaweka nje kwa muda mrefu, bila shaka anguko la timu
hiyo litatokea.
Hali kama hiyo imekuwa
ikiisumbua mara kwa mara Arsenal na ni wazi inajulikana inafeli kutokana na
kukumbwa na lundo la wachezaji majeruhi katika wakati mgumu. Bado mechi 21
kumaliza msimu huu wa Premier, je, Leicester itaweza kuhimili kasi ya vigogo wa
ligi hiyo au ndiyo itakuwa hadithi ya Mtibwa msimu uliopita! Tusubiri tuone mwisho
wao.
IMEANDIKWA NA:
OMARY SULTAN MDOSE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni