Baada ya kupigwa kwa michezo ya mwishoni mwa juma, ukapigwa mchezo mwingine wa Jumatatu December 14 kwenye ligi ya England maarufu kama EPL ambapo Leicester City walikuwa wenyeji wa Chelsea vijana kutoka jijini London.
Leicester City wakazidi kuudhihirishia ulimwengu kwamba wanashikilia usukani wa ligi si kwa kubahatisha kufuatia kuwatoa jasho Chelsea ambao ni mabingwa watetezi wa taji la EPL kwa kuwachapa kwa bao 2-1 na kuitoa Arsenal kileleni mwa ligi.
Mchezaji bora wa ligi hiyo wa mwezi November Jamie Vardy aliendeleza kugawa dozi baada ya kuufungua wavu wa Chelsea dakika ya 34 kipindi cha kwanza kwa kuunganisha pasi ya Riyad Mahrez na kuiandikia Leicester bao la kuongoza ambalo lilidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
Mahrez akathibitisha kwamba yeye ni bora na ni mchezaji wa kiwango cha kimataifa baada ya kutandika bao la pili dakika tatu tu baada ya kipindi cha pili kuanza na kuiacha Chelsea imeduwaa.
Bao hilo lilivuruga mipango yote ya Chelsea iliyokuwa imejipanga kusawazisha goli la kwanza lakini ikajikuta ikiongezewa mlima wa kupanda.
Loic Remy aliyeingia dakika ya 65 kuchukua nafasi ya Oscar akaifungia Chelsea goli la kufutia machozi dakika ya 77 kipindi cha pili akiunganisja krosi iliyopigwa na Rodriguez.
Matokeo hayo yameirejesha tena Leicester City kileleni mwa ligi ya England ikifikisha pointi 35 ikifuatiwa na Arsenal ambao wanapointi 33 wakati Chelsea wakisalia kwenye nafasi ya 16 na pointi zao 15 huku timu zote zikiwa zimeshacheza mechi 16 hadi sasa.
VIBWAGIZO MBALIMBALI VYA MCHEZO HUO
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni