WAKATI leo anatarajiwa kuiongoza timu yake, TP Mazembe katika mchezo wa Klabu Bingwa ya Dunia nchini Japan, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesema safari ya Ulaya imeiva.
Akizungumza kutoka Osaka, Japan jana ambako yuko na TP Mazembe kwa ajili ya Kombe la Dunia, Samatta amesema mipango ya kuhamia Ulaya imekamilika.
“Mipango imefikia katika hatua za mwisho, ila naweza kusema mambo yanakwenda vizuri na wakati ukifika nitasema timu gani ninakwenda,”amesema Samatta.
Samatta na Mtanzania mwenzake, Thomas Emmanuel Ulimwengu leo wanatarajiwa kuiongoza Mazembe katika mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji, Sanfrecce Hiroshima.
Wakati Mazembe imeanzia moja kwa moja Robo fainali, wenyeji hao walilazimika kuitoa Auckland City kwa kuifunga 2-0, mabao ya Yusuke Minagawa na Tsukasa Shiotani katika mchezo wa mchujo.
Mshindi kati ya kikosi hicho cha Hajime Moriyasu na Mazembe mjini Osaka leo, atamenyana na River Plate ya Argentina Desemba 16 Uwanja wa Nagai mjini Osaka katika Nusu Fainali.
Mchezo mwingine leo utazikutanisha Club America ya Mexico na Guangzhou Evergrande ya China na mshindi atakutana na mabingwa wa Ulaya, Barcelona Desemba 17 Uwanja wa Yokohama katika Nusu Fainali.
Mechi za kusaka mshindi wa tatu na fainali zitachezwa Desemba 20 Yokohama.
Samatta, aliyezaliwa Januari 7, mweaka 1992 alijiunga na Mazembe mwaka 2011 akitokea Simba SC, ambayo aliichezea kwa msimu mmoja tu baada ya kuhama African Lyon.
Hadi sasa ‘Sama Goal’ ameifungia Mazembe mabao 60 katika mechi 103 za mashindano yote.
Mdogo huyo wa kiungo wa Mgambo JKT, Mohammed Samatta mwaka jana alikwenda kufanya majaribio CSKA Moscow ya Urusi, ambako bahati mbaya akaumia baada ya siku tatu na kurejea Lubumbashi.
CHANZO:Binzubeiry
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni