Kiungo wa Manchester United, Mjerumani Bastian Schweinsteiger 31, anakabiliwa na adhabu ya kufungiwa mechi tatu na chama cha soka England (FA) kutokana na kitendo chake cha kumpiga kiwiko usoni mlinzi wa Westham United, Winston Reid katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana Jumamosi iliyopita.
Schweinsteiger ana hadi Alhamis hii, saa sita mchana kukubali/kukataa kosa hilo baada ya FA kumuadhibu Jumatatu hii. Refarii Marc Clatternburg aliwaita wachezaji wote wawili na kuongea nao, huku asichukue hatua nyingine yeyote kutokana na kutoona tukio hilo.
Chama cha waamuzi kupitia video wamebaini kosa hilo la Bastian Schweinsteiger lililotokea kabla ya mapumziko na sasa mchezaji huyo anaweza kufungiwa hadi mechi tatu zinazosimamiwa na chama cha soka England, FA.
Habari hizi sio nzuri kwa Manchester United ambayo inakabiriwa na majeruhi ya viungo wake wengine Morgan Schneiderlin na Ander Herrera huku Bastian Schweinsteiger akiwa miongoni mwa watu muhimu katika kikosi hicho hivi sasa.
Kocha wa Manchester United, Louis Van Gaal akizungumzia tukio hilo anasema hakuona chochote na hivyo hana la kufanya zaidi ya kuwaachia wenye mamlaka kutimiza sheria. Kocha wa Westham Bilic amesema kuwa Bastian alistahili kadi nyekundu lakini akasisitiza hawezi mlaumu mwamuzi kwani hakua katika kona nzuri ya kuona tukio hilo.
Beki wa kati wa Westham aliyefanyiwa tukio hilo Winston Reid alisema kuwa Bastian mwenyewe anajua alichomfanyia na hivyo kutokana na mwamuzi kutoona tukio hilo, lakini alistahili kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni