“NINAFIKIRI
miaka 10 niliyoitumikia timu ya Taifa Stars inatosha kiukweli na huu ni
muda wangu sahihi wa mimi kustaafu kuichezea timu hiyo.
“Acha
niwaachie vijana wengine wanaochipukia waje kuichezea Stars kwa
mafanikio makubwa katika kuhakikisha inapata mafanikio katika siku za
baadaye.
“Naamini
ni maamuzi sahihi kwa wakati sahihi kwangu kutangaza kustaafu kuichezea
Stars, ninaamini wapo wachezaji wengi wanaochipukia watakaonirithi mimi
na wakongwe wenzangu,” hizo ni kauli za beki mkongwe wa Yanga, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’.
Cannavaro
ambaye alikuwa nahodha wa Taifa Stars kwa miaka kadhaa, amechukua
uamuzi huo ikiwa ni siku chache baada ya kuvuliwa unahodha wa kikosi
hicho, ambapo cheo hicho kimekabidhiwa kwa Mbwana Samatta anayetarajiwa
kutimkia Ubelgiji kwenda kuichezea Klabu ya Genk ya nchini humo akitokea
TP Mazembe ya DR Congo.
Katika mahojiano maalum na Cannavaro jijini Dar es Salaam, juzi. Mambo yalikuwa hivi;
Sababu ya kustaafu
“Maneno-maneno
naona yamekuwa mengi sana nikiwa naichezea Stars, yalianza mara baada
ya mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia dhidi ya
Algeria kule kwao.
“Katika
mechi hiyo tulifungwa mabao 7-0, kama unakumbuka mechi hiyo muda mwingi
tulicheza pungufu baada ya Mudathiri (Yahya) kutolewa kwa kadi
nyekundu.
“Kiukweli
tulipambana kuhakikisha tunawatoa Algeria lakini ikashindikana, cha
ajabu mara baada ya mechi hiyo nilionekana mimi pekee ndiye
niliyefungisha, sikujisikia vizuri kwa sababu nilipambana kwa ajili ya
taifa langu na mwisho wa siku naonekana si lolote.
Ehee! Amechokwa kumbe
“Kutokana
na minong’ono hiyo iliyokuwa inazungumzwa huku wakitaja umri wangu kuwa
ni tatizo wakidai nimezeeka, nikaanza kufikiria kuwa inatosha. Nikaanza
kupata maoni kuwa niwaachie vijana wenye umri mdogo waendelee kuichezea
Stars.
Sakata la kuvuliwa unahodha
“Sing’ang’anii
na wala silazimishi kuwa nahodha, kikubwa ninachotaka ni kupewa heshima
yangu kwanza kama shujaa niliyeipeperusha vema bendera ya Tanzania kwa
mafanikio hayohayo madogo.
“Kiukweli
nimepokonywa unahodha bila ya heshima, ninajisikia vibaya kupokonywa
unahodha kwa kupitia vyombo vya habari kitu ambacho siyo sahihi, hali
hiyo imeshusha heshima yangu kwa kiwango kikubwa.
“Nilitakiwa
kupewa taarifa kwa maana ya kupewa barua ya kiofisi na TFF (Shirikisho
la Soka Tanzania) na baada ya hapo ingetangazwa kwenye vyombo vya
habari, lakini siyo kama hivi ilivyofanyika, mimi nilipata taarifa za
kuondolewa unahodha na kupewa Samatta kupitia televisheni kitu ambacho
siyo sahihi.
“Nilishangaa
utaratibu huo uliotumika, baada ya kupata taarifa hiyo kupitia
televisheni, siku iliyofuata ndipo Kocha Mkwasa (Boniface) akanipigia
simu na kuniambia kuwa wamempa unahodha Samatta, nikamuitikia tu na
kukaa kimya.
“Hivi
alivyoondolewa unahodha Maxime (Mecky), Swed (Salum) na Nsajigwa
(Shadrack) ni sawa na mimi nilivyoondolewa unahodha? Nimeumia sana,
heshima yangu ipo wapi hapo sasa? Licha ya kulitumikia taifa langu kwa
nguvu na moyo mmoja, leo naonekana si lolote.
Barua ya kustaafu kupelekwa TFF
“Nimepanga
kupeleka barua TFF ya kuwapa taarifa ya kustaafu kwangu kuichezea timu
ya taifa, kwa sababu hali inaonyesha kabisa nimechokwa, hivyo acha
nijiondoe mwenyewe kabla ya kufukuzwa. Sitaki nistaafu kuichezea Stars
kwa dharau kama iliyotokea ya kupokonywa unahodha bila ya kupewa
taarifa.
Abaki na Yanga yake
“Nguvu
zangu zote nitazihamishia katika klabu yangu ya Yanga. Hivi sasa
nimepona majeraha ya enka niliyoyapata nikiwa naitumikia Stars
tulipocheza na Algeria, hivyo ninaamini baada ya wiki mbili nitarejea
uwanjani,” anahitimisha Cannavaro.
SOURCE: CHAMPIONI


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni