MSHAMBULIAJI Kipre Herman Tchetche inadaiwa amesaini klabu ya Al-Nahda Al-Buraimi, Oman, wakati bado ana Mkataba na Azam FC ya Dar es Salaam, Tanzania.
Kiongozi mmoja wa Al Nahda inayoshiriki Ligi Kuu ya Oman, ameposti kwenye akaunti yake ya Twitter picha za Kipre Tchetche akisaini Mikataba na kuandikia; “Muivory Coast Kipre Tchetche rasmi mchezaji wa kwanza wa kigeni Al Nahda ,”.
Kiongozi huyo amechanganya lugha Kiingereza ‘kigumu’ na Kiarabu katika maelezo yake ya kwenye picha.
Na kwa mujibu wa picha hizo, inaonekana Kipre alisaini mikataba hiyo akiwa nyumbani kwake, Kijichi, Dar es Salaam ambako amepangiwa na Azam FC.
KIpre Tchetche akisaini Mikataba inayodaiwa kuwa ya kujiunga na Al Nahda ya Oman |
Pamoja na hayo, Kipre mwenyewe alikana kusaini timu yoyote bali akasema ameamua basi kucheza Tanzania, anataka kwenda kupata changamoto nyingine kwingine.
Akizungumza jana kutoka kwao, Ivory Coast, Kipre alisema kwamba anataka kuzungumza na uongozi wa Azam FC umruhusu kuondoka.
“Inatosha kwa muda ambao nimecheza Tanzania, nahitaji kuondoka kwenda kutafuta changamoto nyingine kwingine.
Nimekuwa na maisha mazuri sana Azam, viongozi na wamiliki wanajali sana wachezaji, lakini nalazimika kuyaacha yote,”amesema.
Kipre ambaye amebakiza mwaka mmoja katika Mkataba wake, amesema kwa sasa yupo mapumzikoni kwao Ivory Coast na anatarajia kuwasiliana na uongozi wa Azam juu ya mpango wake huo.
Wazi kwa kitendo cha kumsaini Tchetche akiwa bado ana Mkataba na Azam, Al Nahda itakuwa ‘imeingia mkenge’ na pia inaweza kuchukuliwa hatua na FIFA.
Na tayari Azam FC imeambatanisha picha za Kipre Tchetche na barua ya malalamiko kupeleka FIFA ikiishitaki Al Nahda na mchezaji mwenyewe – ambao kwa pamoja wanaweza kuadhibitiwa.
PICHA-BINZUBEIRY
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni