Jose Mourinho amewaasa mashabiki wa Manchester United kusahau yote yaliyotokea miaka mitatu iliyopita wakati timu hiyo ilipokuwa chini ya David Moyes na Louis van Gaal na kuangalia namna ya kuirudisha upya katika zama zake.
Mourinho amethibitishwa leo na Man United rasmi kuwa kocha klabu hiyo akichukua mikoba ya Mholanzi Louis Van Gaal baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu.
Mourinho anakabiliwa na mtihani mzito wa kuirudisha United katika zama za ubora wake chini ya Sir Alex Ferguson na kurudisha tena imani kwa mashabiki.
“Tunaweza kuingalia timu yetu katika sehemu mbili,” alisema Mourinho, “sehemu ya kwanza ni miaka mitatu iliyopita na nyingine ni historia inayobeba klabu hii.
“Nadhani ningependa kusahau kilichotokea ndani ya miaka mitatu iliyopita, napenda kuangalia timu kubwa (Man United) ambayo ipo mikononi mwangu kwa sasa na nadhani mashabiki wanachosubiri kusikia kutoka kwangu ni kusema kuwa nataka ushindi.
Nadhani wachezaji wanahitaji kusikia nikisema- hivi, Nataka kushinda”.
“Najisikia vizuri. Nadhani hiki ni kipindi sahihi kuipokea klabu hii kwa sababu ni moja ya vilabu ambayo unahitaji kujiandaa ili kuweza kufanya vyema, ndiyo maana naiita klabu kubwa.
“Na klabu kubwa lazima ipate kocha mkubwa na nadhani mimi ni mmoja wao, hivyo nina furaha sana kupewa jukumu hili, naweza kusema nimefarijika sana kupewa heshima kuwa ya kuifundisha klabu hii”.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni