BARAZA la Wazee la klabu ya Yanga limetangaza msimamo wake wa kumuunga mkono Mwenyekiti wa sasa wa klabu hiyo, Yussuf Manji katika uchaguzi wa klabu hiyo mwezi ujao.
Bado haijajulikana haswa ni lini uchaguzi wa Yanga utafanyika, kutokana na Bodi ya Wadhamini wa Yanga kutangaza Juni 5 na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuagiza ufanyike Juni 25.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam, Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Omar Akilimali amesema kwamba wanamuunga mkono Manji kutokana na mazuri aliyoifanyia klabu.
Akilimali alisema Yanga kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika ni sababu tosha ya kumrejesha madarakani Manji.
Hata hivyo, Akilimali alisema anasikitishwa zimeanza kampeni chafu dhidi ya Manji zinazoendeshwa na watu wasioitakia mema Yanga.
Akatolea mfano suala la kusema vyama vya siasa vya CHADEMA na CCM vimeungana kuhakikisha vinampora Manji umiliki wa ufukwe wa Cocoa, Dar es Salaam ni uzushi. “Tangu lini CCM na CHADEMA wakaungana, huu ni uzushi,”amesema na kuongeza;
“Haya mambo kwa nini yasiibuke siku zote hizo yanakuja kuibuka sasa, hawa watu wana nia gani na Yanga, ninaomba wana Yanga popote nchini wazipuuze habari hizo, si za kweli,”amesema Akilimali.
Akilimali amesema wao kama Wazee wa Yanga hawawezi kupinga na dola kwa lolote dhidi ya Manji, lakini wanaamini habari hizo ni uzushi wenye nia ya kumchafulia Mwenyekiti wao huyo kuelekea uchaguzi ujao.
Pamoja na hayo, Akilimali akawapongeza wachezaji wa Yanga, benchi la ufundi na uongozi chini ya Mwenyekiti, Manji kwa kuiwezesha timu kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Yanga SC ilirejea juzi jioni Dar es Salaam kutoka Angola, ambako Jumatano walikata tiketi ya kuingia hatua makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika licha ya kufungwa bao 1-0 na wenyeji Sagrada Esperanca katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania hatua hiyo Uwanja wa Esperanca mjini Dundo, Angola.
Lakini Yanga wanakwenda hatua ya makundi kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya awali kushinda 2-0 Dar es Salaam, mabao ya Simon Msuva na Matheo Anthony.
Matokeo hayo si tu yanamaanisha Yanga inatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza katika historia yake, bali pia inakuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua hiyo ya michuano hivyo.
Awali ya hapo, Yanga imewahi kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998, ikafuatiwa na mahasimu, Simba SC mwaka 2003.
Ikumbukwe, Yanga iliangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
Yanga ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Yanga inaungana na FUS Rabat, Kawkab Marrakech zote za Morocco, Etoil du Sahel ya Tunisia, Ahli Tripoli ya Libya, MO Bejaia ya Algeria, Medeama ya Ghana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo (DRC) katika hatua hiyo.
Droo ya makundi yote, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho inatarajiwa kupangwa Jumanne ya Mei 24, 2016 makao makuu ya CAF, Cairo nchini Misri saa 6:30 mchana.
Timu zilizofuzu Ligi ya Mabingwa ni Enyimba ya Nigeria, Al Ahly na Zamalek za Misri, AS Vita ya DRC, Asec Mimosas ya Ivory Coast, Wydad Casablanca ya Morocco, ES Setif ya Algeria na Zesco United ya Zambia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni