MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba bila ridhaa yao, beki Hassan Kessy ataanza kuichezea Yanga Agosti mwaka huu kwa mujibu wa utaratibu.
Akizungumza na leo, Hans Poppe amesema kwamba kanuni za usajili ziko wazi na amewatahadharisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoiingiza Yanga mkenge.
“Yanga wakikubali kupotoshwa na wakamtumia Kessy, wajue watakatiwa rufaa na watashindwa. Kwa sababu kanuni zipo wazi, hawapaswi kumtumia, labda kwa ridhaa yetu, au hadi ifike Agosti,”amesema.
Hans Poppe amesema Kessy ataanza kucheza Yanga SC Agosti mwaka huu |
Akifafanua, Poppe amesema kwamba baada ya Kessy kumaliza Mkataba wake Simba SC, anapaswa kusajiliwa na timu nyingine kwa mujibu wa utaratibu wa kalenda ya usajili wa nyumbani.
“Hawawezi kufanya lolote, kanuni ni zao wenyewe TFF, walikopi na kupesti za FIFA. Kwa kifupi ukimsaini mchezaji yeyote yule ambaye bado yupo kwenye Mkataba hata kama umebaki siku moja kwisha, basi lazima upate barua ya timu yake, la hutaki basi subiri usajili ufunguliwe pingamizi ziishe kisha utahalalishiwa,”amesema Poppe na kuongeza.
“Na hawezi kuwa halali hadi itangazwe na Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji mwezi wa nane,”.
Yanga imemsajili Kessy baada ya kumaliza Mkataba wake Simba, lakini ameshindwa kupata leseni ya kucheza michuano ya Afrika hadi awasilishe barua ya kuruhusiwa na klabu yake ya zamani.
Beki Hassan Kessy alikuwa mchezaji wa Simba SC msimu uliopita
Hassan Kessy baada ya kujiunga na Yanga mwezi uliopita na sasa anaambiwa asubiri hadi Agosti kuanza kazi kwa mwajiri mpya
Na Yanga imejaribu kuwaandikia barua Simba kupitia TFF, lakini hadi jana hakukuwa na majibu yoyote.
Tayari Kessy amekosa mchezo wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MO Bejaia nchini Algeria ambako Yanga ilifungwa 1-0.
Na sasa anaelekea kukosa mchezo wa pili wa kundi hilo Jumanne dhidi ya TP Mazembe ya DRC Jumanne Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga kwa sasa ipo kambini mjini Antalya, Uturuki ikijiandaa na mchezo dhidi ya Mazembe na inatarajiwa kurejea Dar es Salaam kesho.
Binzubeiry
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni