MKUTANO WA RAIS WA TFF JAMAL MALINZI NA VYOMBO VYA HABARI KWENYE UKUMBI WA TFF, KARUME STADIUM-ALHAMIS JUNI 30, 2016
NDUGU WANAHABARI
Nimewakaribisha
kuzungumza nanyi kuhusu hali isiyo ya kawaida iliyojitokeza katika
uendeshaji wa mashindano ya kimataifa hususani ushiriki wa Klabu ya
Young Africans katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani
Afrika (CAF Confederation Cup).
Awali ya yote ninaomba nichukue fursa hii kuwapongeza wachezaji,benchi la ufundi pamoja na uongozi wa
klabu
ya Yanga chini ya Rais wao Bwana Yusuf Manji kwa mafanikio makubwa
ambayo klabu yao imepata hadi kufikia hatua ya makundi katika kombe la
Shirikisho la CAF.Kuvunjika koleo sio mwisho wa uhunzi,imani ya TFF ni
kuwa pamoja na kupoteza mechi mbili za mwanzo hatua ya makundi Yanga
bado inaweza kufanya vizuri na kuwa moja ya timu bora mbili katika kundi
lao.
Ndugu
zangu,TFF ndicho chombo chenye jukumu la kuendesha , kuratibu na
kusimamia mashindano yote ya kitaifa na kimataifa ndani ya Tanzania
Bara. Ikumbukwe kwamba mashindano yote ya CAF na FIFA ndani ya Tanzania
msimamizi wake ni TFF.Hii ni kwa mujibu wa Katiba ya FIFA ibara ya
67,Katiba ya CAF ibara ya 59 na Katiba ya TFF ibara ya 12.
Mashindano
yoyote ya kimataifa yanayofanyika nchini Tanzania au kuhusisha timu za
Tanzania ni sharti kibali kiombwe na TFF. Hivyo na ushiriki wa Young
Africans na Azam katika mashindano ya kimataifa msimu wa 2015/2016
ulikuwa na baraka za TFF.
Mamlaka
ya TFF katika mashindano ya ndani na ya kimataifa ni pamoja na
usimamizi wa maandalizi ya mchezo, usimamizi wa mapato,usimamizi na
uhakiki wa haki za matangazo, usalama ndani na nje ya uwanja,usimamizi
wa upelekaji taarifa CAF na FIFA nk Hivyo kwa yeyote anayetaka kucheza
mpira unaotambuliwa na FIFA, CAF, CECAFA na TFF ni sharti akubaliane na
kutii mamlaka hizi.
Pale ambapo Katiba hizi hazielezei moja kwa moja
utaratibu wa uendeshaji wa mashindano husika basi moja kwa moja vyombo
hivi vya mpira huchukua jukumu la kutoa mwongozo.
TFF
inaomba kuchukua fursa hii kuwaomba radhi wadau wote wa mpira na
wapenzi wote wa mpira kwa kadhia yote iliyotokea kutokana na kitendo
cha klabu ya Yanga kutoa tangazo la watazamaji kuingia bure katika
mchezo namba 107 Yanga vs TP Mazembe uliofanyika uwanja wa Taifa Jumanne
tarehe 28 June 2016.
Aidha TFF inachukua fursa hii kuvishukuru vyombo
vya ulinzi na usalama kwa hatua walizochukua ili kuepusha maafa ambayo
yangeweza kutokea. Tunaushukuru uongozi wa Wizara ya
habari,utamaduni,sanaa na michezo kwa ushirikiano wa karibu
waliotupatia wakati wa kuelekea kwenye mechi hii.Shukrani za pekee kwa
Mh Paul Makonda,Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam kwa kufuatilia kwa karibu
matukio yote yaliyohusisha mchezo huu na kuhakikisha unamalizika salama.
Sasa ninaomba
turejee kwenye matukio yaliyozunguka maandalizi ya mechi hii.Young
Africans, wakiwa na wawakilishi wao katika mkutano wa maandalizi wa
Alhamisi Juni 23, 2016 kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
walitangaza juu ya kuchapisha tiketi 40,000 na wakatangaza na
viingilio.TFF baada ya kikao hicho iliwajulisha CAF juu ya jambo hili
kama ilivyo ada.
Mkutano
wa kawaida wa maandalizi ya mechi (pre match meeting) baina ya timu
zote mbili,yaani Yanga na TP Mazembe ulifanyika tarehe 27 June 2016
katika ukumbi wa hoteli ya Coral Beach, Masaki jijini Dar es Salaam na
uliendeshwa na Mratibu Mkuu wa CAF wa mchezo huo (General coordinator) ,
Sidio Jose Magadza – Raia wa Msumbiji.Ni katika kikao hiki Yanga
walitamka kuwa wameamua kiingilio kitakuwa ni bure.Msimamizi wa CAF
alikiambia kikao kuwa kama hayo ndiyo maamuzi ya Yanga watambue kuwa
itakuwa ni kwa gharama zao.
Aidha aliagiza watazamaji 40,000 tu ndio
waruhusiwe kuingia uwanjani hata kama ni bure,hii ni kwa sababu za
kiusalama.Hilo halikufanyika na badala yake uwanja ulijaa watu
60,000. Na kutokana na pilika pilika za watu kutaka kuingia uwanjani
zilitokea vurugu ambazo ilibidi wanausalama wazitulize kwa nguvu.
Hili
nalo lilishuhudiwa na wawakilishi wa CAF na hatujui wameripoti vipi
tukio hili.Ikumbukwe wajibu wa TFF, CAF na FIFA ni kuhakikisha
mashindano yao yanafanyika kwa utulivu na amani bila kuathiri maisha ya
watu,mali zao na miundombinu ya michezo.
Ndugu zangu,ninaomba nihitimishe kwa kuzungumzia yafuatayo.
1. Serikali
kupitia msimamizi wa uwanja wa Taifa ambaye ni Wizara ya habari
Utamaduni Sanaa na michezo tarehe 27 June 2016 iliandika barua TFF
ikitoa kibali cha uwanja kutumika kwa mechi ya Yanga vs TP Mazembe kwa
masharti kuwa miundo mbinu ya uwanja isiathirike,tozo na maduhuli
(entitlements) ya Serikali yalipwe na usalama wa watazamaji ulindwe.TFF
inawasiliana na mamlaka husika ikiwemo Wizara,mamlaka ya mapato pamoja
na CAF ili kujua ni kiasi gani wanatakiwa kulipwa.Hili likisha fahamika
basi TFF itachukua jukumu lake kama msimamizi wa mpira nchini
kuhakikisha kila mwenye kudai analipwa.
2. TFF
inafuatilia kwa karibu kujua nini yatakuwa maamuzi ya CAF kutokana na
ripoti za msimamizi na kamisaa wa mchezo kuhusu matukio yaliyotokea nje
ya uwanja kabla na wakati wa mechi.
3. TFF
itaendelea kufanya kila lililo katika uwezo wake kuhakikisha Yanga
inaendelea kufanya vizuri kwenye mashindano haya kwani bado ina nafasi.
4. Siku
zote TFF imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha mchezo wa mpira
unachezwa katika eneo salama.Hivyo kuanzia sasa jukumu la kusimamia
michezo ya kimataifa litakuwa linaratibiwa kwa karibu zaidi na TFF ikiwa
ni pamoja na mapokezi ya timu,maofisa,kuangalia malazi kama yako
sahihi,usalama,maamuzi kuhusu viingilio na uuzaji wa tiketi,usafiri wa
ndani,viwanja vya mazoezi nk.
Ninaomba
nimalizie kwa kuwatakia tena ndugu zetu Waislam ibada njema ya Mwezi
Mtukufu wa Ramadhan,niitakie pia kila la kheri timu yetu ya Serengeti
Boys ushindi katika mchezo wa marudianao Jumamosi dhidi ya Seychelles.
Michezo ni furaha,michezo ni afya.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Jamal Malinzi
Dar es Salaam
30 June 2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni