WAKALA wa nyota wa Slovakia Marek Hamsik amekaririwa akisema kuwa mchezaji huyo ataendelea kusalia Napoli licha ya tetesi zinazoendelea kuwa atajiunga na Chelsea au Manchester United.
Timu zote zilionesha nia ya kumtaka mchezaji huyo mwenye miaka 28 tangu miezi kadhaa iliyopita huku akiwa katika kiwango bora kwenye michuano ya Euro 2016. Pamoja na hayo wakala wake Juraj Venglos amekanusha haraka taarifa za mchezaji huyo kujiunga na miamba hiyo ya Uingereza.
Venglos ameiambia Radio Crc: "Hamsik tayari yupo kwenye klabu kubwa haoni sababu ya kuondoka.
"Siku chache zijazo nitakutana na Rais Aurelio De Laurentiis na Mkurugenzi wa michezo Cristiano Giuntoli, lakini siwezi kuzungumzia mustakabali wa nyota huyo ila hawezi kwenda popote."
Wakati huo huo Hamsik mwenyewe akizungumza na Sky Italia, alisema ataongeza mkataba wa kuendelea kubaki na hafikirii kwenda mahali popote.
“Naipenda hii jezi, siku zote nimekuwa nikisema hivyo, bado nina miaka mitano zaidi ya kuendelea kubaki hapa, nina furaha na nitaebdelea kuwepo,” alisema Hamsik.
Hamsik alionyesha kiwango kizuri katika ushindi wa magoli 2-1 wa nchi yake dhidi ya Urusi na Jumatatu atakiongoza kikosi hicho kumenyana na Uingereza katika muendelezo wa michuano ya Euro.
TETESI YA PILI;
JUVENTUS inahitaji dau la kuvunja rekodi ya dunia la pauni 160 milioni toka Real Madrid ili kumuachia kiungo wake Paul Pogba katika dirisha hili la usajili.
Kocha wa Madrid Zinedine Zidane na Rais Florentino Perez wamemfanya kiungo huyo kuwa mchezaji wao namba moja msimu huu sambamba na mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya ufaransa Dimitri Payet.
Los Blancos wanatarajia kumuuza James Rodriguez ili kupata fedha ya kumchukua Pogba, lakini bei hiyo inaweza kutibua dili hilo huku kiungo huyo pia akiwindwa na Manchester United, Manchester City, Chelsea na Paris Saint Germain.
Gazeti la Marca la nchini Hispania limeripoti kuwa Madrid haitokuwa tayari kutoa kitita hicho kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23 huku wakala wake Mino Raiola akisema dili hilo litakamilika.
Ripoti zinasema kuwa Juve wanajua Real hawana longo longo katika matumizi ya pesa hasa wanapo muhitaji mchezaji kama walivyowauzia Zidane mwaka 2011 kwa kuvunja rekodi ya dunia ya wakati ule lakini katika hili miamba hiyo ya Hispania inaweza ikachemka.
Zidane ni shabiki mkubwa wa kiungo huyo kitu kinachoipa Real nafasi ya kupata saini yake huku wote wakitokea taifa la Ufaransa.
Pogba kwa sasa yupo na kikosi cha Ufaransa kinacho shiriki michuano ya Euro na tayari ameshaisaidia kupata ushindi wa michezo yake yote miwili ya awali.
TETESI YA TATU;
MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Leicester City, Aiyawatt Srivaddhanaprabha anaamini mshambuliaji wao anayewindwa na Arsenal Jamie Vardy ataendelea kusalia Kings Power msimu ujao baada ya kuipiga chini ofa ya Washika bunduki hao.
Arsenal walipeleka ofa ya pauni 20 milioni ambayo walikuwa na matumaini ya kukamilisha dili hilo kabla ya kuanza kwa michuano ya Euro 2016. Vardy alichelewa kutoa maamuzi hadi itakapomalizika michuano na sasa klabu yake imempandishia mshahara hadi pauni 100,000 kwa wiki sawa na ambao angelipwa Arsenal.
Akizungumza na gazeti la Mail, Makamu huyo alisema hatma ya mshambuliaji huyo itajulikana muda mfupi ujao na ana uhakika wa kumbakiza mpachika magoli huyo aliyetisha msimu uliopita.
"Mtapata habari muda si mrefu, lakini nina imani atabaki.
Tunataka kujenga kikosi bora msimu ujao kitakacho washangaza wengi kuanzia kwenye ligi na klabu bingwa.
"Michuano ya klabu bingwa tumepania kufanya vizuri japokuwa wengi wanatuona kama ni wachanga, na hatutishiki na uchanga wetu," alimaIizia Aiyawatt.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni