YANGA SC imewasili salama mjini Bejaia, Algeria mchana wa leo, tayari kwa mchezo fungua dimba wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika Jumapili dhidi ya wenyeji, Mouloudia Olympique Bejaia.
Yanga imefikia katika hoteli ya kifahari ya Raya mjini humo na leo baadaye itafanya mazoezi Uwanja wa jirani, kabla ya kesho kufanya mazoezi Uwanja wa Unite Maghrebine ambao utatumika kwa mchezo wa Jumapili.
Yanga imewasili kutoka mjini Antalya, Uturuki ambako iliweka kambi katika hoteli ya Rui tangu Jumapili.
Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Morocco, Bouchaib El Ahrach atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.
Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma anatarajiwa kuiongoza timu yake dhidi ya MO Bejaia Jumapili |
Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A.
Na katika mchezo huo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa kutoka nchi tatu tofauti, ambao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.
Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao utachezeshwa na marefa wa Shelisheli Bernard Camille, Hensley Danny Petrousse na Eldrick Adelaide.
Kikosi kamili cha Yanga kilichopo kambini Uturuki ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya.
Mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Vincent Bossou na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Viungo; Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya.
Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.
Msafara upo chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa Mohammed Mpogolo na Meneja Hafidh Saleh.
WAKATI HUO;
KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Obrey Chirwa amewasili jioni ya leo Dar es Salaam tayari kukamilisha usajili wake kujiunga na Yanga SC.
Chirwa alikuwa mshambuliaji pacha wa Donald Ngoma katika klabu ya FC Platinums ya Zimbabwe.
"Amewasili muda huu, ndiyo nimempokea, tunakwenda kumalizana naye sasa,"amesema Kaimu Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit .
Na baada ya Ngoma kuhamia Yanga, akawashauri viongozi wa timu hiyo wamchukue winga huyo wa kulia wa timu ya vijana ya Zambia chini ya umri wa miaka 23.
Obrey Chirwa akiwa kwenye gari la Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam wakielekea makao makuu ya klabu, ambako anatarajiwa kusaini Mkataba wa miaka miwili
Na inaaminika Yanga imekubali kutoa zaidi ya dola za Kimarekani 100 000 kuipata saini ya Chirwa ambaye anatokea FC Platinum ya Zimbabwe, klabu waliyotokea wachezaji wake wengine, Wazimbabwe Thabani Kamsuoko na Ngoma.
Mwaka jana, Chirwa alikataa kujiunga na Hobro IK ya Denmark kwa kutoridhishwa na malipo - na maana yake Yanga itakuwa imempa mshahara mzuri.
Yanga inataraka kutuma jina la mchezaji huyo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ili awahi kucheza mechi za Kundi A Kombe la Shirikisho.
Na mpango huo utafanywa mapema tu atakapokamilisha usajili wake leo akiwasili.
PICHA NA BINZUBEIRY
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni