RATIBA ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2016/17 imetoka rasmi Julai 19, mwaka huu ambayo ni siku moja baada ya kuvuja kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Ratiba iliyovuja kwenye mitandao, ilikuja kukanushwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lililodai kwamba ile ya mitandaoni ilikosewa Anuani ya Posta ya TFF, lakini pia ilionyesha mchezo kati ya Azam FC dhidi ya African Lyon ungechezwa Agosti 21, 2016 wakati hii waliyoitoa wao ilikuwa na anuani sahihi ya shirikisho hilo na mchezo huo wa raundi ya kwanza ukionyesha utachezwa Agosti 20, 2016.
Hilo limepita, lakini wengi wamejiuliza maswali kwa nini ratiba ivuje kwanza kisha ndiyo ije kutolewa hadharani siku inayofuata.
Kwa mujibu wa TFF, ratiba waliyoitoa imezingatia michuano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa ngazi ya klabu na timu za taifa ili kukwepa dhana yoyote ya upangaji wa matokeo na kurundikana kwa michezo. Wanahitaji pongezi kwa kuliona hilo, lakini ni je, hayo waliyoyasema ni ya kweli!
Ukiangalia kwa umakini utagundua kuna matatizo ndani ya ratiba hiyo ambayo ni yaleyale kwa kila msimu yanayolalamikiwa lakini hayafanyiwi kazi.
Kiporo cha Yanga vs JKT Ruvu
Kosa la kwanza ni hili, ligi kuanza tu kuna kiporo cha mchezo mmoja ambao ni Yanga vs JKT Ruvu. Msimu uliopita timu kama Simba ilitangaza kugomea kupeleka timu uwanjani wakishinikiza timu ya Yanga iliyokuwa na viporo vingi wacheze kwanza ili wawe sawa. Kulikuwa na mvutano mkubwa sana.
Lakini pia duniani kote tunafahamu kwamba msimu wa ligi ukianza, basi timu zote zinapaswa kucheza siku ya kwanza au kwa mfano baadhi zinacheza leo na zingine kesho.
Katika ratiba yetu hiyo ya msimu unaokuja inaonyesha Agosti 20, mwaka huu ndiyo msimu unaanza, na siku hiyo zitapigwa mechi saba na moja kuwekwa kiporo. Mechi hiyo ni ile itakayowakutanisha mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga dhidi ya JKT Ruvu.
Sababu ambazo ziliainishwa za kuupeleka mbele mchezo huo ni kutokana na Yanga kukabiliwa na michuano ya kimataifa ambapo Agosti 23, mwaka huu yaani siku tatu baada ya kuanza kwa ligi, wao watatakiwa kuwa DR Congo kucheza dhidi ya TP Mazembe kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi.
Kwa kutambua kwamba Yanga inakabiliwa na mchezo wa kimataifa siku chache baada ya kuanza kwa ligi, ingetumika busara msimu wa ligi kuanza angalau Agosti 27, mwaka huu ili timu zote zicheze siku hiyo na siyo kama ilivyo kwa kuanza tu na kiporo ambacho kinakuja kuchezwa siku ya 11 mbele.
Mapinduzi Cup haijapewa nafasi
Kila mwaka, kumekuwa na michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo hufanyika visiwani Zanzibar kwa takribani wiki mbili kuanzia Januari Mosi mpaka 12.
Kwa misimu ya nyuma, ratiba ya ligi kuu inapopangwa husahaulika kuwekwa ‘gape’ kupisha michuano hii hali inayopelekea ligi kusimama, kumbuka kuwa wiki chache inakuwa imetoka kusimama kutokana na kumalizika kwa mzunguko wa kwanza na kupisha kipindi cha usajili.
Kutokana na kila msimu kuibuka lawama kwa nini inatokea hali hiyo, tulitarajia ratiba ya msimu ujao itakuwa na ‘gape’ kupisha michuano hiyo kama ilivyofanyika katika mechi za Kombe la FA, timu za taifa, pamoja na michezo ya kimataifa kwa timu za klabu.
Ukiiangalia ratiba yenyewe, Januari Mosi, mwakani kuna mechi mbili za kumalizia raundi ya 17 baada ya mechi sita za raundi hiyo kupigwa Desemba 31, mwaka huu.
Januari 7 na 8, mwakani kutakuwa na mechi nane za raundi ya 18 kabla ya Januari 14 na 15 kupigwa mechi nane za raundi ya 19 ambapo mechi hizo zitapigwa ikiwa zimepita siku kama mbili au tatu baada ya kumalizika kwa Kombe la Mapinduzi. Hakuna ubishi, hapa lazima ligi itasimama tena kwa wiki mbili baada ya mzunguko wa kwanza kumalizika Novemba 6, mwaka huu.
Mechi mbili za mwisho hazijapangiwa siku ya kuchezwa
Tunafahamu kwamba Yanga na Simba zimekuwa na kawaida ya kuutumia Uwanja wa Taifa uliopo jijini Dar es Salaam kwa michezo yao ya nyumbani ambapo pia msimu ujao ratiba inaonyesha hivyo kwa timu hizo kuutumia uwanja huo.
Lakini kwa kulitambua hilo, wapangaji wa ratiba ambao ni Bodi ya Ligi Kuu Bara Tanzania (TPBL), wamepanga mechi za mwisho za kuhitimisha msimu wa 2016/17 kuchezwa Aprili 8, mwakani.
Katika mechi hizo za mwisho, ratiba inaonyesha zitapigwa sita badala ya nane, mechi mbili ambazo ni Simba vs African Lyon na Yanga vs Prisons, hazijapangiwa siku yake wakati imezoeleka mechi za mwisho kama hizo kuchezwa siku moja na muda mmoja kuepuka michezo ya upangaji matokeo.
Ratiba inaonyesha Simba na Yanga zitawakaribisha wapinzani wao kwenye Uwanja wa Taifa, hali ambayo inaleta maswali itakuaje mechi mbili kupigwa kwenye uwanja mmoja, ina maana wahusika hapa hawakujua mapema namna ya kufanya ili kuondoa utata huu, tusubiri tuone.
mdosejr@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni