STORI YA KWANZA;
BEKI mpya wa Simba SC, Hamad Juma aliyeanguka bafuni mwishoni mwa wiki nyumbani kwake na kulazwa hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam, anaendelea vizuri.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara amesema leo kwamba beki huyo wa kulia anaendelea vizuri baada ya matibabu ya takriban saa 24.
“Anaendelea vema na ndani ya siku mbili kuanzia kesho anaweza kuruhusiwa kurudi nyumbani. Tunamshukuru Mungu,”amesema Manara.
Hamad Juma (kushoto) katika mchezo dhidi ya Ndanda FC, hapa anamtoka Salum Telela |
“Baada ya kukimbizwa hospitali alifanyiwa uchunguzi wa kina na kisha kupatiwa tiba, ikiwemo kushonwa nyuzi kadhaa, ila hali yake inaendelea vema kwa sasa,”alisema Manara.
Tayari Hamd Juma amefanikiwa kuwa beki chaguo la kwanza wa kulia wa Simba SC, mbele ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog baada ya kucheza vizuri mechi mbili zilizopita dhidi ya URA katika sare ya 1-1 na dhidi ya Ndanda FC katika ushindi wa 3-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na kwa ajali hii, wazi Hamad atakosekana katika mchezo ujao dhidi ya JKT Ruvu Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
STORI YA PILI;
KOCHA Mmalawi wa Mbeya City, Kinnah Phiri amesema kwamba walikosa bahati tu ya kufunga mabao wakitoa sare ya 0-0 jana na wenyeji Kagera Sugar Uwanja wa Kambarage, Shinyanga katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Phiri alisema timu yake ilicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi, lakini ikashindwa kumalizia tu kwa kufunga na wazi ilikosa bahati katika mchezo huo.
“Tulicheza vizuri, hatukuwa na bahati, mapungufu kadhaa tumeayaona tutayafanyia kazi ili tuweze kuibuka na matokeo zaidi kwenye micheo inayofuata, asanteni sana mmefanya vizuri”.
Kocha Phiri wa kwanza kushoto katika benchi la Mbeya City kwenye moja ya mechi za msimu uliopita
City ilianza dakika 45 za mwanzo kwa mashambulizi makali ikimiliki eneo la kiungo lilokuwa chini ya Kenny Ally na kufakikiwa kulifikia mara kadhaa lango la Kagera Sugar, lakini umakini kwenye safu ya ushambuliaji ulihitimisha dakika hizo za mwanzo timu zote zikiwa 0-0.
Kipindi cha pili kocha Kinnah Phiri alifanya mabadiliko ya kuwatoa, Joseph Mahundi, Rajabu Isihaka na Salvatory Nkulula na nafasi zao kuchukuliwa na Michael Kerenge, Ramadhani Chombo na Ditram Nchimbi mabadiliko ambayo yalikuja kuongeza ushai safu ya ushambuliaji lakini mpaka dakika 90 zinakamilika hakukuwa na bao lolote.
Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu, Simba SC iliichapa Ndanda FC 3-1 Uwanja wa Taifa, Azam ililazimishwa sare ya 1-1 na African Lyon Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Ruvu Shooting iliifunga 1-0 Mtibwa Sugar uwanja wa Mabatini Mlandizi, Pwani na Stand United ikalazimishwa sare ya 0-0 na Mbao FC Uwanja wa Kambarage Jumamosi Prisons ikashinda ugenini 1-0 dhidi ya Maji Maji Uwanja wa Maji Maji, Songea.
Ligi Kuu itaendelea Jumatano kwa Toto Africans kuikaribisha Mwadui Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, wakati Jumamosi Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa Ndanda FC Uwanja wa Manungu, Morogoro, Azam wataikaribisha Maji Maji na Prisons watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Mechi nyingine za Jumamosi, Mbao watakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Kirumba, Mwanza, JKT Ruvu watamenyana na Simba Uwanja wa Taifa, Kagera Sugar watamenyana na Stand United Uwanja wa Kambarage, wakati mabingwa watetezi, Yanga SC watacheza mechi ya kwanza Jumapili kwa kumenyana na African Lyon, siku ambayo pia Toto Africans watakuwa wenyeji wa Mbeya City Kirumba, Mwanza.
STORI YA TATU;
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Mspaniola Zeben Hernandez Rodriguez amesema kwamba Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itakuwa ngumu na anahitaji muda zaidi kutengeneza timu ya ushindi wa uhakika.
Rodriguez amesema kuwa anahitaji muda zaidi ili kukisuka kikosi chake na kucheza kupitia mifumo wanayoendelea kuwafundisha wachezaji wa timu hiyo.
Kocha huyo wa zamani wa Stanta Ursula ya Hispania, alisema ameshuhudia mechi za kwanza za ligi msimu huu na kudai kuwa haitakuwa ligi rahisi sana na ngumu kwake yeye kutokana na kikosi alichonacho.
Zeben Hernandez Rodriguez (katikati) amesema kwamba Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itakuwa ngumu
“Cha muhimu ni wachezaji kuendelea kushika mifumo yangu ninayoendelea kuwafundisha, kwa uzoefu wetu tuliokuwa nao hapa tumegundua timu yoyote inayocheza na Azam hata timu iwe kibonde vipi, basi itajitahidi kuweza kuweka rekodi, hili si tatizo sana tutaendele kupambana nalo kwa kuwa hii ni kazi yetu,” alisema.
Kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, kitaanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Majimaji kesho Jumanne asubuhi, mechi itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex, Jumamosi ijayo saa 10.00 jioni.
Zeben pia ametanabaisha kuwa atayafanyia kazi makosa yote yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya African Lyon ulioisha kwa sare ya 1-1, ili waweze kufanya vizuri mchezo ujao dhidi ya Majimaji.
“Kwa sasa tunafanya tathimini ya mchezo uliopita, kutoa makosa na kurekebishana pale tulipokosea, tukimaliza hapo kwa wiki hii tutaanza kujipanga kwa mchezo ujao (Majimaji), lakini cha kwanza tunaangalia yali yaliyotokea katika mchezo wa kwanza, mapungufu yalikuwa wapi na nani anapaswa kufanya nini,” alisema.
Azam FC kwa sasa ni miongoni mwa timu zilizoko nafasi ya nne hadi ya tisa kwenye msimamo wa ligi, zote zikiwa zimekusanyia pointi moja kila mmoja zikizidiwa pointi mbili na vinara Simba, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons, walijikusanyia pointi tatu.
Akizungumzia mchezo wa kwanza dhidi ya African Lyon, Zeben alisema timu yake haikucheza vibaya sana kulingana na mechi zilizopita huku akidai kuwa tatizo kubwa linalokikabili kikosi chake ni ufungaji wa mabao.
“Hilo si tatizo sana kadiri muda utakavyokuwa ukienda, hali itabadilika, ni jambo la kuvuta subira na muda zaidi, ukipatikana muda wa kutosha basi timu itakuwa vizuri zaidi mpaka sehemu ya ushambuliaji,” alisema.
Mbali na hilo amesema kuwa wiki hii, atalifanyia kazi suala la wachezaji wake kushindwa kumaliza mechi kipindi cha kwanza, akidai kuwa kwa mechi kadhaa zilizopita kikosi chake kimekuwa kikitafuta ushindi kipindi cha pili kuliko mwanzoni mwa mechi.
“Sikuwa na timu mwanzo, nimeingia kikosini hivi sasa na nimeanza kubadilisha mfumo na mbinu kwa timu kucheza namna tunavyotaka sisi kulingana na mifumo, hilo ni tatizo ambalo lipo ni kubwa kwa sasa na tunaendelea kujitahidi kulifanyia kazi na hata wiki hii tutaendelea nalo ili kwa mechi zijazo liweze kuondoka,” alisema.
Zeben aliendelea kusema kuwa jambo linaloonekana hivi sasa ni timu zote zinazokuja Azam Complex kucheza na timu yake, hufanya jitihada kubwa kuliko uwezo wao ili kuonyesha nao wanaweza kucheza mpira.
“Hili si tatizo kubwa sana inabidi tuendelee kulizoea na nitaendelea kuiboresha timu, ili kwa yoyote atakayekuja Chamazi au nje ya Chamazi tuweze kumfunga,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni