Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Mwenyekiti wake, Wakili
Richard Sinamtwa, imemtaka beki wa Yanga, Hassan Kessy kuilipa klabu yake ya
zamani, Simba SC shilingi Milioni 120 kwa kuvunja Mkataba.
Kessy ametakiwa kuilipa klabu yake ya zamani,
Simba SC kiasi hicho cha fedha ili aanze kuichezea timu yake mpya, Yanga
katika mashindano kuanzia sasa.
Habari za ndani kutoka TFF zimesema kwamba Kamati
imejiridhisha kwamba Kessy alivunja mkataba na Simba kinyume cha utaratibu
hivyo anapaswa kuilipa Simba.
Habari zaidi zinasema kwamba, katika mkataba wake
na Simba, wote klabu na mchezaji walikubaliana atakayevunja mkataba huo atalipa
Dola za Marekani 60,000sawa na zaidi ya Shilingi Milioni 120,000 za
Tanzania.
Kessy alisajiliwa na Simba SC misimu miwili
iliyopita kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa Mkataba wa miaka miwili akilipwa
Shilingi Milioni 20.
Naye Meneja wa Kessy, Athumani Tippo
amesema anashangazwa na uamuzi wa Kamati hiyo kumtaka Kessy ailipe Simba.
Tippo amesema mkataba wa Kessy na Simba uliisha
tangu Juni 17 na beki huyo wa kulia akasaini Yanga SC Juni 21, baada ya
kuzungumzo ya awali kufanyika mwishoni mwa Mei.
“Kilichotokea ni kuwa baada ya habari za Kessy
kutaka kuhamia Yanga kuvuja, Mei 25 mwaka huu alipokwenda kwenye mechi ya
fainali ya Kombe la TFF dhidi ya Azam mashabiki wakamvisha jezi ya Yanga,”
ameongeza.
Amedai kuwa hakuvishwa jezi hiyo na klabu ya
Yanga bali ni mashabiki hivyo huwezi kusema Kessy alivunja mkataba na Yanga
kinyume cha utaratibu.
Hatahivyo, Meneja Tippo amesema kwamba
amepeleka malalamiko Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA) ili waweze
kumsaidia mchezaji huyo katika sakata hilo.
Yanga tayari wameweka msimamo wa kutokuwa tayari
kulipa Shilingi Milioni 120 ambazo Simba wanataka ili Kessy aichezee klabu hiyo
yenye maskani yake Mtaa wa Jangwani ikimaanisha kuwa kuna uwezekano beki huyo
akakaaa jukwaani na kutazama mpira kama shabiki wa Yanga.
Chanzo: Hivi sasa
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni