STORI YA KWANZA;
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba hana shida kurejea Yanga, iwapo klabu hiyo itafuata taratibu za kumuomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza jana, Mkwasa alisema kwamba amesikia
taarifa za kutakiwa kurejea Yanga, lakini hajazipokea rasmi kutoka kwa
uongozi wa klabu hiyo.
Na
hata hivyo, Mkwasa alisema kwa kuwa yeye ana Mkataba na TFF wa
kufundisha timu ya taifa – basi uongozi wa Yanga utalazimika kufuata
taratibu ili kumpata.
“Mimi sina tatizo na Yanga. Ndiyo imenifikisha hapa, nikianza kuitumikia kama mchezaji na baadaye kocha. Na nilikuja Taifa Stars nikitoka Yanga. Hivyo sina shida kabisa kurudi kule, ia wafuate tu taratibu kama kweli wananitaka. Waongee tu na TFF,”alisema.
Kocha
Mkuu wa sasa wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm yupo katika wakati
mgumu kufuatia timu kuambulia pointi 11 kati ya 18 za mechi sita za Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba hana shida kurejea Yanga, iwapo klabu hiyo itafuata taratibu
Yanga SC imetoa sare mbili, imefungwa mechi moja na kushinda tatu tangu kuanza kwa Ligi Kuu – hiyo ikiwa ni mbali na kupoteza mchezo wa Ngao ya Jamii mbele ya Azam kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 2-2.
Na baada ya mchezo wa Jumamosi wakilazimishwa sare ya 1-1 na mahasimu, Simba SC waliokuwa pungufu kwa sehemu kubwa kufuatia Nahodha wao, Jonas Mkude kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 29, baadhi ya viongozi wa Yanga wamependekeza mwalimu huyo aondolewe.
Kamati ya Utendaji ya Yanga inaweza kukutana wiki hii kujadili benchi la Ufundi la timu kwa ujumla, baada ya malalamiko mengi kuhusu kuporomoka kwa kiwango cha timu na wachezaji, ingawa Kaimu Katibu wa klabu, Baraka Deusdedit alisema jana kwamba hadi sasa wana imani na Pluijm.
Habari zaidi zinasema Pluijm amekuwa akilalamikiwa hadi na Wasaidizi wake na viongozi wa Kamati ya Mashindano kwamba hataki ushauri.
Pluijm pia analalamikiwa kushauri wachezaji ambao wanaonekana bado kuhitajika katika timu kama Salum Telela waachwe na kupendekeza kusajiliwa kwa wachezaji ambao mwishowe hawatumii kama Obrey Chirwa.
Pluijm alisaini Mkataba mpya wa miaka miwili Julai mwaka huu baada ta kuiwezesha timu kushinda mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
Hata hivyo, Pluijm aliyeiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola, kuanzia hapo akashindwa kuendeleza matokeo mazuri kwenye mechi za timu hiyo.
Yanga ilifungwa mechi nne kati ya sita za Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika.
Ilifungwa na mbili za TP Mazembe 1-0 Dar es Salaam, 3-1 Lubumbashi, ikafungwa 3-1 na Medeama SC Ghana na 1-0 na MO Bejaia mjini Bejaia, Algria, wakati yenyewe ilishinda mchezo mmoja tu dhidi Bejaia 1-0 Dar es Salaam na kutoa sare ya 1-1 na Medeama Dar es Salaam.
Ikumbukwe Pluijm alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2014, akirithi mikoba ya Mholanzi mwenzake Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts, lakini mwisho wa msimu Juni akaondoka kwenda Al Shoalah FC ya Saudi Arabia pamoja na aliyekuwa Msaidizi wake, Charles Boniface Mkwasa.
Yanga SC ikamuajiri Mbrazil Maximo, ambaye baada ya miezi mitano akafukuzwa kufuatia kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Simba SC Desemba 13, 2014 na Pluijm akarejeshwa kazini hadi sasa.
CHANZO; BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
STORI YA PILI;
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limesema kwamba halitambui klabu ya Yanga SC kukodishwa kwa kampuni ya Yanga Yetu, kwa kuwa taratibu haazikufuatwa na Baraza la Wadhamini la klabu hiyo halitambuliki.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa BMT, Mohammed Kiganja amesema kwamba wao wanaendelea kutambua kama Yanga SC ni mali ya klabu na haijakodishwa kwa kampuni ya Yanga Yetu.
Kiganja amesema kwamba, taratibu hazikifuatwa katika mchakato mzima ulioifikisha Yanga SC kwenye kukodishwa, hivyo zoezi hilo ni batili.
“Hatupingi klabu zetu kufanya mabadiliko isipokuwa tunajaribu kuwakumbusha kufuata utaratibu wa kisheria na katiba zao. Kwa sababu unapobadilisha jina au kufanya marekebisho yoyote, ni lazima vikasajiliwe na kutambulika,”amesema.
Aidha, Kiganja amesema hata Baraza la Wadhamini wa Yanga lilipitisha uamuzi wa kuikodisha timu, haitambuliki kwa Msajili wa Vyama na Klabu na Michezo wa BMT, kwa Wajumbe wake wengi ni wa muda.
Amesema kati ya Wajumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga lililoundwa Julai 5, mwaka 1973 ni wawili tu wanaotambulika na walio hai hadi sasa, ambao ni Dk. Jabir Idrisa Katundu na Juma Mwambelo, wakati wengine wamekwishafariki dunia.
“Mwembelo pamoja na kwamba bado yupo hai, lakini kwa muda sasa hahusishwi tena mambo yanayoendelea ya klabu hiyo,” amesema.
Kiganja amewataja Wajumbe wengine wa Baraza hilo la Muda, ambalo halikuwahi kusajiliwa wala kupitishwa kwenye Mkutano Mkuu ni Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, Mama Fatuma Karume, Francis Kifukwe, Amri Ramadhan, Juma Kambi na Abeid Mohammed.
Na akasema ili Yanga ikodishwe, inazotakiwa kwanza kifanyike kikao cha Kamati ya Utendaji itakayochambua hoja na kukubaliana au kutokukubaliana kabla ya kwenda kwenye Mkutano Mkuu wa wanachama, uwe wa dharura au kawaida na maamuzi yatakayofikiwa katika Mkutano yatapelekwa Baraza la Wadhamini, ambalo ndilo litawasilisha suala hilo kwa Msajili.
“Sheria ya BMT ya mwaka 1967 kifungu namba 11 (1) kinasema chama chochote kinachofanya mabadiliko ya jina, anuani, madhumuni au kifungu chochote cha katiba yake kitatakiwa idhini ya Msajili.
Kifungu namba 11 (3) Msajili anaweza kuyakataa maombi ya kubadili kifungu chochote cha Katiba kama ataona kuwa mabadiliko yanaweza kuhatarisha usalama na kuvuruga amani, au kama kuna malengo ya kuwanufaisha wachache au kama hayazingatii sera za michezo na sheria za BMT,” amesema Kiganja.
Katibu huyo wa BMT amesema kwamba mchakato huo wa Yanga kukodishwa ungekuwa halali tu kama taratibu hizo zingefuatwa na kupita kote.
STORI YA TATU;
WATAALAMU wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), wanatarajiwa kutua nchini wakati wowote kuanzia sasa kwa ajili ya kukagua Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Huu ni utaratibu wa CAF ambako baada ya muda hutembelea nchi wanachama kuangalia maendeleo ya miundombinu ya mpira wa miguu kabla ya kupandisha hadhi ya viwanja kwa ajili ya michuano ya kimataifa inayosimamiwa na kuendeshwa na CECAFA, CAF na FIFA.
Ukaguzi huo unafanyika wakati Tanzania inasubiri majibu ya Uwanja wa Sokoine wa Mbeya ambao ulikwiisha kukaguliwa na mapendekezo ya uboreshwaji kutolewa ili uweze kupandishwa hadhi ya matumizi ya kuchezwa mechi kubwa kama vile fainali za Kombe la Shirikisho, Ngao ya Hisani, michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mechi kubwa za kimataifa za kirafiki na mashindano ya CECAFA, CAF na FIFA.
Viwanja ambavyo CAF na FIFA inavitambua nchini Tanzania hadi sasa ni Amani wa Unguja, Zanzibar; Kaitaba wa Kagera, Azam Complex na Uwanja Mkuu wa Taifa vya Dar es Salaam.
Endapo CCM Kirumba utapitishwa, kutakuwa na nafasi ya kuruhusu kuchezwa mechi kubwa kama vile fainali za Kombe la Shirikisho, Ngao ya Hisani pamoja na mechi kubwa za kimataifa za kirafiki na mashindano ya CECAFA, CAF na FIFA.
Kirumba inaingia kwenye orodha ya viwanja vya Gombani ulioko Pemba; Sokoine wa Mbeya, Kaitaba wa Kagera ambavyo vilikwisha kukaguliwa na sasa vinasubiri kupitishwa ili kutumika kimataifa. Ujio wa viwanja hivyo, utapanua wigo wa Tanzania kuandaa michuano mikubwa katika ngazi ya timu za taifa kimataifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni