KAMATI ya bodi ya ligi Uendeshaji na Usimamizi umeipiga faini klabu ya Simba ya shilingi milioni tano na kuiagiza ilipe fedha za ukarabati wa viti kutokana na uharibifu uliofanywa na mashabiki wa timu hiyo wakati wa mchezo wa ligi kuu ya Vodacom dhidi ya mahasimu wao Yanga mtanange uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Oktoba mosi.
Kamati hiyo iliyoketi jana imemuondolea adhabu ya kadi nyekundu kwa nahodha wa timu ya Simba Jonas Mkude baada ya kujiridhisha bila mashaka kuwa mchezaji huyo hakustahili kupewa kadi hiyo.
Mbali na ripoti ya kamishna wa mchezo huo uliooneshwa moja kwa moja kwenye luninga kamati inaendelea na uchunguzi kuhusu uchezeshaji wa mwamuzi Martin Saanya na wasaidizi wake Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha kabla ya kutoa maamuzi mengine dhidi yao endapo itathibitika kuwa walifanya makosa kwenye mchezo huo.
Ofisa Habari wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Alfred Lucas alisema Kamati hiyo inaendelea na uchunguzi kuhusu mechi mbali mbali za ligi kuu na kuzitolea maamuzi ya haraka.
"Kumekuwa na taarifa za upotoshaji zinatolewa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu suala hilo la mechi ya Simba na Yanga, lakini hii ndiyo rasmi kutoka ndani ya kamati" alisema Lucas.
Kamati hiyo pia imempiga faini Msemaji wa klabu ya Simba Hajji Manara ya shilingi laki mbili kwa kosa la kuingia uwanjani licha ya kutokuwa miongoni mwa maofisa waliotakiwa kuwepo eneo hilo.
Wakati huo huo klabu ya Azam imepigwa faini ya shilingi milioni tatu baada ya kuvaa nembo ya mdhamini wa ligi mkono mmoja badala ya miwili kwa mujibu wa kanuni za ligi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni