NDANDA FC imekata Rufaa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupiga klabu ya Simba kuwachezesha wachezaji wawili wa kigeni, kipa Daniel Ayei na kiungo James Kotei katika mchezo wa jana baina yao.
Katibu wa Ndanda, Suleiman Kachele ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba wameikatia rufaa Simba kwa kuchezesha wachezaji ambao hawakuwa na vibali vya Idara ya Uhamiaji.
“Sisi tumekata Rufaa kwa kuwa Simba iliwachezesha wachezaji ambao hawakuwa na vibali na sasa tunasubiri matokeo, ila matarajio yetu haki itatendeka tutapewa pointi tatu,”alisema Kachele.
Simba SC iliwafunga wenyeji, Ndanda mabao 2-0 katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Kipa Daniel Ayei anadaiwa kuidakia Simb SC bila kuwa na kibali cha Uhamiaji
Na katika mchezo huo, wachezaji wa Ghana, kipa Agyei na kiungo Kote walicheza mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu baada ya kusajiliwa dirisha dogo.
Agyei alicheza hadi filimbi ya mwisho, wakati Kotei alitolewa baada ya dakika 19 tu kufuatia kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Muzamil Yassin aliyekwenda kufunga bao la kwanza na kuseti la pili lililofungwa na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim kipindi cha pili.
Lakini kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alisema kwamba taratibu zote zilifuatwa ili kuwachezesha wachezaji hao.
“Wao Ndanda wasifikiri sisi Simba ni watu wa mchezo mchezo tuwachezeshe bila vibali. Acha wapeleke rufaa yao Bodi, watapewa majibu huko,”alisema Kaburu.
Siku mbili kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu, TFF ilizionya klabu zote zilizosajili wachezaji wa kigeni au makocha katika dirisha dogo kutowatumia kwenye mechi za Ligi Kuu hadi wapatiwe vibali vya kufanya kazi nchini kutoka Idara ya Uhamiaji.
TFF pia kwa kutumia kanuni ya 72 ya Ligi Kuu ya Vodacom ilizitaka klabu kuhakikisha makocha wake wote wana sifa ambazo ni kuwa na leseni B au A ya CAF.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni