HATIMAYE kitendawaili cha uwanja utakaotumika kwa fainali ya michuano ya kombe la FA kati ya timu za Simba na Mbao FC kimeteguliwa na sasa mtanange huo utapigwa kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Kitendawili hicho kimeteguliwa na Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF) Jamal Malinzi wakati wa ufunguzi wa kozi ya awali ya makocha na waamuzi iliyoandaliwa na chama cha soka wilaya ya Ubungo muda mfupi uliopita.
Hapo jana Rais Malinzi kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika kuwa kungefanyika droo ya kupata uwanja kwa ajili ya fainali hiyo hivyo kukazuka mijadala mikubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uhahali wa jambo hilo kutokana na kanuni za michuano hiyo kutoanisha kuhusu taratibu za kupata uwanja kwa ajili ya fainali.
Malinzi alisema “Natangaza rasmi fainali ya michuano ya kombe la FA kati ya Simba kutoka Dar es Salaam na Mbao kutoka Mwanza itafanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma ili kupata usawa wa pande zote.”
Mchezo huo wa fainali umepangwa kufanyika Mei 28 huku ikielezwa kuwa matengenezo ya uwanja wa Taifa yanayoanza Mei 21 yamechagiza maamuzi haya kwavile hautokuwa tayari kwa matumizi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni