Mabingwa watetezi Dar Young Africans wameuvunja mwiko wa kutokufungwa Kwa timu ya soka ya Azam msimu huu baada ya kuwachapa kwa mabao 2-1 kwenye mchezo muhimu wa raundi ya 15 ya ligi kuu soka Tanzania Bara.
Kadhalika katika mchezo huo ambao umefanyika katika uwanja wa Azam Complex ulipo Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, imekuwa ni mara ya kwanza kwa Azam kuruhusu kufungwa mabao mawili wanapokuwa katika uwanja wao wa nyumbani.
Mpira ulianza kwa kasi kwa kila timu kujaribu kuucheza na kuumiliki mpira ili kuleta madhara langoni mwa mpinzani wake.
Azam hawakuwachelewesha sana mashabiki wake kuwapa burudani Kwani dakika ya nne tu Mpira ulioanzia kwa Bruce Kangwa kulia mwa lango la Yanga ukamkuta Shabani Idd Chilunda naye bila ajizi akapiga shuti lililomshinda kipa Youthe Rostand na kujaa wavuni.
Baada ya bao hilo Yanga walitulia na kuanza kutengeneza mashambulizi lakini ngome ya Azam ilikuwa imara, hilo likawafanya kuanza kupiga mashuti ya mbali na dakika ya 15 shuti la Papy Kabamba Tshishimbi lilitulia vyema mikononi mwa kipa Razak Abalora.
Yanga hawakukata tamaa, pasi ya Ibrahim Ajib ilikwenda moja kwa moja hadi kwa Obrey Chirwa ambaye alikutana wangu wangu na Razak Abalora aliyejaribu kuuokoa mpira lakini ukapenya na bila ajizi Chirwa akamalizia na kuandika bao la kusawazisha kwa Yanga, ikiwa ni dakika ya 30 ya mchezo.
Baada ya bao hilo Yanga walitulia zaidi na kuanza kumiliki mpira jambo ambalo lilimfanya kocha Aristica Cioaba kufanya mabadiliko kwa kumtoa Bernard Arthur na kumuingiza Salmin Hoza ili kuweka uhai eneo la kiungo lililoonekana kumilikiwa vilivyo na Yanga.
Dakika ya 44 Azam wakidhani Yanga wamepoa kutokana na mabadiliko yao, Gadiel Michael Mbaga aliachia shuti kali kwa guu lake la kushoto na kwenda moja kwa moja wavuni, kuandika bao la pili kwa upande wa Yanga.
Mpaka timu zinakwenda mapumziko Yanga walikuwa kifua mbele kwa mabao mawili huku Azam ambao ndio wenyeji wa mchezo huo wakitoka na bao moja.
Kipindi cha pili Azam waliingia wakiwa tofauti kidogo ambapo kwenye Dakika ya 58 almanusura Azam waandike bao la kusawazisha lakini kukosekana kwa umakini kwa mchezaji Enock Atta Agyei kukaifanya Yanga kuendelea kuongoza, kwani shuti lake lisilokuwa na macho likatoka nje na kuwa goal kick.
Dakika ya 81 mwamuzi Israel Mjuni Nkongo alimzawadia kadi ya pili ya njano na kuwa nyekundu kiungo Salum Abubakar kwa kumsukuma Hassan Ramadhan Hamis.
Hadi kipyenga cha mwamuzi Israel Mjuni Nkongo kinapulizwa kuashiria kukamilika Kwa dakika 90 Yanga walitoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-1.
Ushindi huo unawafanya Yanga kuendelea kushika nafasi ya tatu wakiwa na alama 28 wakati Azam wakisalia katika nafasi ya pili wakiwa na alama 30.
Walioanza Yanga: Youthe Rostand, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Andrew Vicent, Kelvin Yondani, Juma Makapu, Rafael Daudi, Papy Tshishimbi, Obrey Chirwa, Ibrahim Ajibu/Juma Mahadhi na Emanuel Martin/Geofrey Mwashiuya.
Akiba Yanga: Ramadhani Kabwili, Haji Mwinyi, Edward Makka, Juma Mahadhi, Saidi Mussa, Mateo Antony na Geoffrey Mwashiuya.
Walioanza Azam: Razack Abalora, Himid Mao, Bruce Kangwa, Agrey Moris, Yakubu Mohamed, Stephan Kingue/Mbaraka Yusuph Abeid, Joseph Mahundi, Salum Abubakar, Bernard Arthur/Salmin Hoza, Shabani Chilunda/Paul Peter na Enock Atta.
Akiba Azam: Mwadini Ally, David Mwantika, Abdallah Kheri, Salmin Hoza, Idd Kipagwile, Mbaraka Yusuph Abeid, Paul Peter.
Kadi za njano.
Azam: Shabani Idd Chilunda dakika ya 10, Salumu Abubakar dakika ya 22, Stephan Kingwe dakika ya 43.
Yanga: Papy Tshishimbi dakika ya 75.
Kadi Nyekundu: Salum Abubakar 'Sure Boy' dakika ya 81.
Matokeo mengine.
MwaduiFC 2 - 2 Njombe Mji (Claide Wigenge, Etiene Ngiladjoe| Salim Hamis, Awesu Awesu).
Kagera Sugar 0-0 Lipuli FC.
Mbeya City 0-0 Mtibwa Sugar.
Mechi za Jumapili.
Simba SC Vs Majimaji
Singida United Vs Tanzania Prisons
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni