Mchezaji wa zamani wa Simba Dua Said akamatwa tuhuma wizi wa maji
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla (kulia), akimhoji mchezaji wa
zamani wa Simba, Dua Said ambaye alikuwa miongoni mwa watu watano
waliokamatwa kwa tuhuma za kujiunganishia maji isivyo halali kutoka
kwenye mabomba ya Mamlaka ya Maji Safi na Taka (Dawasa), kwenye nyumba
zao zilizopo Bonde la Mto Msimbazi, Kigogo, Dar es Salaam. Makalla
alikuwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maji Dar es Salaam. (picha na
Kamanda wa Matukio)
Mchezaji huyo alikamatwa jana wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala, aliyeongozana na wabunge wa Chadema, John Mnyika, Halima Mdee na Suzan Lymo katika operesheni ya dharura ya kuwasaka wezi wa maji katika wilaya ya Kinondoni.
Hata hivyo, mbunge wa Kinondoni, Idd Azan ambaye eneo lake ndilo walilokamatwa watuhumiwa hao, hakuwapo katika ziara hiyo.
Mbali na Dua Said, pia nyumba ya mchezaji wa zamani Nico Bambaga, ambaye kwa sasa ni marehemu ilikutwa imeunganishwa katika mtandao huo wa wizi wa maji sambamba na nyumba zingine tatu.
Akizungumza baada ya kukamatwa, Dua alisema nyumba iliyokutwa imeunganishwa na mfumo huo wa maji katika eneo la Kigogo ni mali yake na kwamba kwa sasa hakai hapo baada ya kuhamia Kinyerezi.
Alisema kuwa kabla ya kuondoka Kigogo alikuwa ni miongoni mwa wajumbe wa kamati ya maji waliokuwa wakipambana na mfumo wa wizi wa maji na kwamba yeye hauzi maji bali anapeleka kwenye nyumba yake nyingine.
"Niliomba kuunganishiwa maji kihalali na sikuyapata mpaka ninaondoka Kigogo ndiyo maana jana nilipoambiwa nije kuna tatizo sikusita kuja," alisema Dua.
Akizungumza baada ya kuwakamata watuhumiwa hao, Makala alidai kuwa Dua alikuwa akivuna maji kiasi cha lita 90,000.
"Moja ya vitu vinavyochangia tatizo la maji ni hili la wizi wa maji, watu hawa kwa ujanja wao wameikosesha serikali mapato pamoja na kuwafanya wananchi wengi wakose maji, lazima wachukuliwe hatua stahiki," alisema.
Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine mengi ya Tanzania yamekuwa katika tatizo sugu la huduma ya maji kwani huduma inayotolewa hailingani na mahitaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni