Aliyekuwa beki wa zamani wa Coastal Union, Abdi Banda (kushoto) amesaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Simba sc
WEKUNDU wa Msimbazi wamefanikiwa kumsajili beki wa
kushoto wa Coastal Union Abdi Banda baada ya kumuweka kwenye rada zake kwa muda
mrefu.
Nyota huyo kinda mwenye uwezo wa kucheza nafasi
zote za ulinzi, lakini beki ya kushoto ndio mahala pake haswaa , alisaini
mkataba wa miaka mitatu jana na mara moja atajiunga na kikosi cha Simba
kinachofanya mazoezi chini ya kocha mkuu, Mcroatia, Zdravko Logarusic.
Banda aliwahi kuripotiwa kuwindwa na Yanga katika dirisha
dogo la usajili mwaka huu, lakini ilishindikana kwasababu alikuwa na mkataba na
wagosi wa kaya na viongozi wa klabu hiyo walilalamika kitendo cha wanajangwani
kumrubuni kijana huyo.
Banda aliwahi kuhojiwa na mtandao huu baada ya
kumalizika kwa michuano ya ligi kuu Tanzania bara msimu uliopita na alikiri
wazi kuwa anatamani kuichezea Simba ingawa alikuwa njia panda kwasababu Yanga
nao walimtangazia dau kubwa.
Banda alijipatia umaarufu kwa aina ya uchezaji
wake na mpaka kuitwa kikosi cha timu ya Taifa chini ya miaka 20, na kama
ataendelea kujitunza katika misingi na nidhamu ya mpira, ni miongoni mwa
wachezaji wanaoweza kulisaidia Taifa siku za usoni.
Ikiwa katika harakati zake za kujiimarisha na
kurudisha makali yake, Simba tayari imeshawasajili wachezaji kadhaa wa nafasi
tofauti.
Tayari imewasainisha makipa wawili, kinda Peter
Manyika na kipa bora wa ligi kuu msimu uliopita, Hussein Sharrif ‘Iker Casillas’
kutokea kwa wakata miwa wa Mtibwa Sugar.
Pia imeshanasa mabeki Jerome Mvengere, Mohammed
Hussein ‘Tshabalala’.
Siku za karibuni, klabu hiyo pia iliwasajili
kiungo mshambuliaji aliyekuwa anaichezea Mtibwa Sugar msimu uliopita, Shaaban
Kisiga ‘Malone’ na mshambuliaji kutoka Ruvu Shooting, Elias Maguri.
Kwasasa Simba inakamilisha taraibu za kuwasajili
wachezaji wawili wa kimataifa, Mkenya
Paul Kiongera na Mrundi Pierre Kwizera na tayari wachezaji hao walishagusa
ardhi ya bongo na kilichobakia ni kumalizana nao vipengele binafsi.
Kama itafanikiwa kuwasainisha wachezaji hao, Simba
itakuwa imekamilisha nafasi tano za wachezaji wa kigeni kwasababu tayari inao
watatu ambao ni mabeki Mganda George Owino ‘Gella’ na Mkenye Donald Mosoto
pamoja na mfungaji bora wa ligi kuu msimu uliopita, Mrundi, Amiss Tambwe.
Hata hivyo, kamati ya usajili bado inahaha kuangaza
kurunzi yake huku na kule ili kuongeza wachezaji wazawa ambapo siku za nyuma,
ilielezwa kuwa kocha mkuu, Logarusic alipendekeza asajiliwe, Antony Matogolo na
Deus Kaseke kutoka Mbeya City fc.
Pia siku za karibuni kulikuwa na taarifa za
usajili wa utata wa mshambuliaji wa Mbeya City fc, Saady Kipanga, ingawa mpaka
sasa hakuna taarifa rasmi kutoka klabuni.
Lakini kipanga ni mchezaji wa Mbeya City na amebakiza mwaka mmoja na nusu, hivyo hakuna bishara ambayo ingefanyika bila kuwahusisha wagonga nyundo hao wa Mbeya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni