Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Mchezaji
bora wa dunia mara mbili Mreno Cristian Ronaldo amekuwa akiimwagia sifa
Manchester United mara kwa mara licha ya kwamba yeye kwa sasa ni mali
ya Klabu ya Real Madrid ya Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).
Jambo hilo pia limejitokeza kwa mshambuliaji Mganda Dan Sserunkuma
ambaye leo amemwaga wino wa kuitumikia klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi,
Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Sserunkuma imethibitishwa rasmi na uongozi wa Simba SC kwamba atakuwa
miongoni mwa wachezaji wapya wa Simba watakaoikabili Yanga SC katika
mechi ijayo ya ‘Nani Mtani Jembe 2′ dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam Desemba 13 baada kusaini mktaba wa miaka
miwili wa kuwatumikia wanamsimbazi.
Sserunkuma, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) alitua jijini jana
usiku na kusaini mkataba huo mbele ya Rais wa Simba, Evans Aveva baada
ya mkataba wake na Gorl Mahia ya KPL kumalizika.
Mara tu baada ya kusaini mkataba huo utakaomuweka Msimbazi hadi Desemba
3, 2016, Sserunkuma ameimwagia sifa mabingwa wa Kenya, Klabu ya Gor
Mahia kwa kumlea vizuri katika miaka miwili na nusu aliyoitumikia.
Amesema Gor Mahia itazidi kubaki moyoni mwake huku akiwamiminia sifa
mashabiki wa klabu hiyo kwa kumuunga mkono katika kipindi chote
alichokuwa na klabu hiyo pamoja na wakala wake, Ken Joseph na familia
yake.
“Nilifurajia maisha ya miaka miwili na nusu Gor Mahia, lakini huu ni
wakati sahihi wa kusema kwa heri. Tulikuwa na nyakati nyingi za kufurahi
na za mafanikio ya pamoja, na mashabiki walikuwa wakiniunga mkono sana –
hasa tulipokuwa katika wakati mgumu.
“Gor Mahia itabaki kuwa moyoni mwangu na ninamshukuru kila mtu ndani ya
menejimenti ya klabvu hiyo kwa kunipa nafasi nyingi za mafanikio
kuonesha kipaji changu.
“Pia ninaishukuru familia yangu na wakala wangu kwa sapoti yao kubwa
kwangu. Sasa ninaangalia mbele kufungua ukurasa mwingine wa maisha yangu
– nikiichezea Simba,” amesema Sserunkuma.
Akiwa Gor Mahia, Sserunkuma alitwaa taji la Ligi ya Timu Nane nchini
Kenya (Top 8 Cup), Ngao ya Hisani na ubingwa wa KPL mara mbili mfululizo
huku akiibuka mfungaji bora wa ligi hiyo msimu huu (2014).
Sserunkuma atakuwa na faida ya kucheza pamoja na Mganda mwenzake Okwi
katika safu ya ushambuliaji ya Simba baada ya kuondolewa kwa Kiongera
ambaye anakwenda India kufanyiwa upasuaji wa goti aliloumia baada ya
kugongana na kipa Shaban Kado wa Coastal Union katika mechi yao ya
kwanza ya sare ya bao moja msimu huu wa VPL kwenye Uwanja wa Taifa
Septemba 21.
Sserunkuma aliyezaliwa Desemba 14, 1989 (umri wa miaka 24 ambao hata
hivyo, una utata kwa wanaofuatilia kwa kina soka la Afrika Mashariki)
jijini Kampala, Uganda amekuwa katika kiwango cha juu tangu ajiunge na
Gor Mahia 2012 akitokea Nairobi City Stars.
Simba wanaamini mkali huyo wa kufumania nyavu atakuwa na msaada mkubwa
katika kikosi chao ambacho kimeonekana kuwa butu msimu huu kikiwa
kimefunga mabao nane tu katika mechi saba za VPL, idadi ambayo ni sawa
na mabao yote ya Tambwe katika mechi saba (akicheza sita) za mwanzo wa
msimu uliopita wa ligi hiyo.
Mbali na Kiongera na Sserunkuma, Simba ina nyota wengine wanne wa kigeni
ambao ni Waganda Emmanuel kwi na Joseph Owino pamoja na Warundi Amissi
Tambwe na Pierre Kwizera.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni