DUBAI
- Rais wa UEFA Michel Platini amesisitiza mpango wake wa kuanza
matumizi ya 'Kadi Nyeupe' itakayowafanya wachezaji watolewe nje kwa muda
kisha kurejeshwa baadaye.
Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 59 alitoa wazo hilo kwa mara ya kwanza Oktoba lakini likapingwa na Rais wa FIFA Sepp Blatter.
Hata hivyo, Platini ameshikilia msimamo wake katika mkutano wa tisa wa kimataifa wa michezo unaofanyika Dubai.
"Kadi nyeupe ni kitu kipya. Inahusiana na tabia ya wachezaji wa soka.
Kujiangusha na kujifanya kuumia, kupinga maamuzi ndani ya uwanja, haya
hayakubaliki kwa watu wanaopenda mchezo.
"Kadi ya njano itaendelea kutumika pia lakini inavutia zaidi kuwa na kadi nyingine.
"Hii kadi nyeupe itamtoa mchezaji ndani ya uwanja kwa dakika kadhaa,
kama tano au 10. Hii itasaidia kuufanya mchezo upendwe na watu
wasiopenda kitendo husika.
"Tukiwa na kadi nyeupe, hakutakuwa na kufukuzwa uwanjani. Ninafikiri
tunapaswa kujifunza kwenye michezo mingine, kama 'rugby', ambao
wanatumia mfumo huu."
Mchezaji huyo wa zamani wa Nancy, Saint-Etienne na Juventus, ambaye
aliiongoza Ufaransa kutwaa ubingwa wa Ulaya 1984 na kutinga mara mbili
nusu fainali za Kombe la Dunia, amesemaSheria ya Kuotea (Sheria Namba 11
ya Soka) inapaswa kurahisishwa ili ieleweke kwa watu wengi zaidi.
"Kuna aina na taratibu nyingi za kuotea. Ni vigumu kupata aina moja na
isiyokiuka miiko kutafsiri sheria ya kuotea. Inabidi tuwaruhusu watu
walioko mbele ya kamera kujua kuotea pia," ameongeza Platini.
"Sasa tunahitaji kuishawishi FIFA".
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni