Na Saleh Ally
TABIA za beki mkongwe wa
Chelsea, John Terry, ni kupenda kujitambulisha kwa washambuliaji anaokutana nao
wakati timu yake ikiwa uwanjani.
Nahodha huyo wa Chelsea
amekuwa akifanya hivyo mara nyingi ikionekana kutaka kumtawala mapema kabisa
kisaikolojia mshambuliaji anayemkaba kwamba ajue amekutana na kiboko yake au
beki katili na asiyetaka mchezo na kazi yake.
Wakati akiwa Liverpool,
mshambuliaji Fernando Torres aliwahi kusema kila walipokutana na Chelsea
alifanya juhudi kubwa kuhakikisha anafunga kwa kuwa alitaka kumuonyesha Terry
ambaye hakufurahishwa na ubabe wake mara kwa mara.
Huenda mara kadhaa, Terry
amekuwa akibadili mbinu zake, lakini hiyo ni moja ya kubwa alizonazo. Wakati
fulani, mpango huo wa Terry ulifeli.
Katika mechi ya kwanza ya
nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Atletico Madrid, Terry alianza mapema
mipango yake ya kutaka kumuonyesha mshambuliaji Diego Costa kwamba yeye ni
nani. Lakini majibu yalikuwa makali kuliko alivyotegemea na ndipo akagundua
kuwa Costa ni namba nyingine na huenda mfumo alioutumia kwa mara ya kwanza
haukuwa sahihi.
Kitendo cha Costa
kuwakanyaga mabeki Emre Can na Martin Skrtel wa Liverpool kimewafanya wengi
waamshe mjadala wa mshambuliaji huyo raia wa Hispania mwenye asili ya Brazil.
Maswali yamekuwa ni mengi,
kama kweli anafaa kuichezea Chelsea, kama kweli wanastahili kuwa na mchezaji
mkatili hivyo. Mwisho wengi wanahoji vipi awe mjeuri namna hiyo? Ingawa
wanavutiwa na uwezo wa kazi zake maana ndiye anaongozwa kwa kutikisa nyavu
katika Ligi Kuu England.
Costa ni mtoto wa
Uswahilini, amekulia maisha hayo na hakuwahi kuishi maisha ya mafunzo ya soccer
kwenye ‘academy’ kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa Ulaya.
Ubabe wa mechi za mchangani
ambazo alikuwa maarufu sana, bado uko kwenye damu yake, ndiyo maana anawapa tabu
sana Wazungu.
Costa alizaliwa katika mji
mdogo wa Lagarto katika Jimbo la Sergipe nchini Brazil. Miaka yote alikuwa
akicheza soka la mchangani na alikuwa maarufu sana.
Hadi alipofikisha miaka 16,
ndiyo alichukuliwa hadi jijini Sao Paulo na kujiunga na timu iliyokuwa na
mafunzo sahihi ya mchezo wa soka.
Waliocheza naye soka katika
Mji wa Lagarto kabla hajaondoka kwenda Sao Paulo, wanasema alikuwa mjeuri, mtu
mwenye hasira na hakuwa na woga hata kidogo.
Lakini kituko cha kumpiga
mchezaji halafu akakimbilia kumsukuma na kumghasi mwamuzi kilikuwa maarufu
zaidi. Baadaye Costa alifungiwa miezi minne. Wakati huo alikuwa akiichezea
Barcelona Esportiva Capella.
Aliwahi kubatizwa jina la
Picardia, neno hilo la Kihispania lenye maana ya mpiganaji au mtu asiye na hofu
na ndivyo anavyoonekana.
Hii inaonyesha kiasi gani
uchezaji wa kibabe Costa hautakwisha na ataendelea kuwa namna hiyo kwa kuwa
hakucheza soka la mafunzo linalomuonyesha afanye vipi kuonekana ni mwenye
nidhamu.
Takwimu zinaonyesha hata kabla
ya msimu kwisha, ameshasababisha tafrani za kawaida mara 22, amekwidana na
mabeki mara tano, amewasukuma kwa kifua mara 13, amewasukuma kwa mikono mara 15
na amekutana na mabeki uso kwa uso na kutoa maneno ya kibabe mara 11.
Pamoja na kwamba ameshakutana
na adhabu kutoka FA, lakini haimbadilishi yeye kuwa alivyo na wengi wamekuwa
wakisema ni zawadi nzuri kwa mabeki wa England ambao wengi wamekuwa wababe kwa
washambuliaji.
Mara kadhaa, Costa ameonekana akiwa amechaniwa jezi au bukta.
Lakini amekuwa akionyesha sehemu alizoumizwa na viatu vyenye njumu za chuma za
mabeki hao ambao sasa wameanza kulalamika.
Hakuna ubishi tena unaweza
kusema ubabe wa Costa ni dawa ya mabeki wababe wa England na karibu kila mchezo
amekuwa akizozana nao na mara nyingi kuwafanya wadau wa soka kuwaonea huruma
mabeki.
Kwa zaidi ya miaka 20,
hakuna aliyewahi kulalamika mabeki wa Ligi Kuu England wamekuwa wakionewa hadi
Costa alipotua England. Je, ataendelea hivyo hadi mwisho?
Mabao anayofunga anaonyesha
ana uwezo na hilo alilidhihirisha Hispania kabla ya kutua England. Je, kuna
mengi anafunga baada ya kuwatisha mabeki?
Jiulize, mabeki wa England
hasa wale wa kati ambao wengi ni wakatili, wataendelea kumvumilia na kushitaki
bila ya kumtafutia dawa?
Ila ukweli, mtoto wa Uswahilini
anawapa shughuli mabeki hao licha ya wao kutamba kwamba England ndiyo kwa
wababe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni