WAZEE
wa Darajani, Mjini London, England, Chelsea The Blues wametoka sare ya
bao 1-1 na wenyeji wao Paris-Saint Germain, PSG, katika mechi ya kwanza
ya hatua ya 16 ya ligi ya mabingwa barani Ulaya iliyomalizika usiku huu
uwanja wa Parc des Princes, nchini Ufaransa.
Kikosi
hicho cha kocha mwenye maneno mengi, 'The Special One' Jose Mourinho
kilianza kuandika bao la kuongoza katika dakika ya 36' kipindi cha
kwanza kupitia kwa beki wake mahiri Branislav Ivanovic.
Hadi dakika 45' za kipindi cha kwanza zinamalizika, Chelsea walikuwa kifua mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili, wenyeji waliingia kwa kasi na kutengeneza mipango ya kusawazisha bao hilo.
Endison
Cavani aliandika kimiani bao la kusawazisha katika dakika ya 54' na
mpaka dakika 90' zinamalizika, timu hizo zimetoka sare ya 1-1.
Takwimu za mchezo huo zinaonesha kuwa PSG wamecheza vizuri zaidi ya Chelsea wakimiliki mpira wa asilimia 53 kwa 47.
Wakali hao wa ligi ya Ufaransa walipiga mashuti 8 yaliyolenga lango dhidi ya 1 la Chelsea.
PSG
wamepiga kona 7 dhidi ya 1 ya Chelsea na hii inaonesha wazee hao wa
Darajani waliingia kwa lengo la kujilinda zaidi kuliko kushambulia.
Imekuwa utamaduni wa Jose Mourinho kupaka basi ugenini, lakini mara nyingi mbinu yake hii humnufaisha.
Chelsea
wanasubiri mechi ya marudiano uwanja wa Stamford Bridge na watahitaji
suluhu (0-0) ili wasonge mbele kwa faida ya goli la ugenini au ushindi
wa aina yoyote ile mfano 1-0.
Katika
mechi nyingine iliyopigwa usiku huu uwanja wa Arena Lviv nchini
Ukraine, Shakhtar Donetsk wametoka suluhu (0-0) dhidi ya wageni Bayern
Munich.
Bayern walitawala mchezo huo na mpaka dakika 90' zinamalizika waliongoza umiliki wa mpira kwa asilimia 59 kwa 41.
Lakini walipiga mashuti 2 tu yaliyolenga lango dhidi ya 1 la wenyeji.
Cha kushangaza zaidi wenyeji hawakupiga kona yoyote ndani ya muda wote wa mchezo, wakati Wakali wa Bundesliga walipiga kona 4.
Hata hivyo, Bayern walifanya madhambi mengi zaidi, mara 19 dhidi ya 14 ya wenyeji wao.
Kwa matokeo hayo, Bayern wanahitaji ushindi wowote katika uwanja wao wa Allianz Arena ili kusonga mbele hatua ya robo fainali.
Bahati mbaya zaidi, Bayern walipata pigo dakika ya 65' kufuatia kiungo wao mkongwe Xabi Alonso kuoneshwa kadi nyekundu.
Michuano hiyo inaendelea leo (februari 19, mwaka huu) kwa mechi mbili kupigwa.
Basel wako nyumbani kukabiliana na FC Porto, wakati Schalke 04 wanawakaribisha mabingwa watetezi, Real Madrid.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni