Simba imeutumia vyema uwanja wake wa nyumbani kwa kuibuka na ushindi wa goli 4-0 mbele ya Mgambo JKT kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa jioni ya leo.
Emanueli Okwi aliyekuwa nyota wa mchezo wa leo, alianza kufunga goli la kwanza dakika ya saba, Ramadhani Singano ‘Messi’ akafunga goli la pili dakika ya 15 akipiga mpira wa adhabu ndogo uliokwenda kujaa moja kwa moja kwenye nyavu za goli la Mgambo JKT.
Dakika ya 39 Okwi akafunga goli la tatu akitumia makosa ya walinzi wa Mgambo waliojichanganya na kumfanya Okwi kufunga goli kwa urahisi, goli hilo liliifanya Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa magoli 3-0 mbele ya wageni wao Mgambo JKT.
Kipindi cha pili Simba walianza mchezo kwa kasi wakifanya mashambulizi kadhaa ya kushtukiza, Okwi ambaye leo alikuwa mwiba mkali kwa Mgambo alifunga goli lake la tatu (Hat-trick) na bao la nne kwa Simba SC dakika ya 51 kipindi cha pili.
Simba wamefanikiwa kulipa kisasi kwa Mgambo JKT kufuatia kupoteza mchezo wa raundi ya kwanza kwa kipigo cha bao 2-0 mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga
Dakika 20 za mwisho timu zote zilicheza kwa tahadhari kubwa kufuatia mvua kubwa kunyesha na kusababisha hali ya uterezi kwenye uwanja, hivyo wachezaji walikuwa wakicheza kwa tahadhari kuzuia makosa yanayoweza kusababishwa na uterezi.
Ushindi wa leo unaiongezea Simba pointi na sasa wamefikisha pointi 38 wakiwa wameshacheza michezo 23 na wanasalia nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC wenye pointi 42 wakiwa nafasi ya pili baada ya mechi 22 wakati Yanga wao wapo kileleni kwa pointi zao 49 baada ya kushuka dimbani mara 22.
Kikosi cha Simba kilichaoanza: Ivo Mapunda, Kessy Ramadhani, Mohamed Hussein, Joseph Owino, Jurko Mursheed, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Said Ndemla, Emanuel Okwi, Ibrahim Hajibu na Awadh Juma.
Kwenye benchi: Denis Richard, Nassoro Masoud, Issa Rashid, William Lucian, Simon Sserunkuma Elius Maguri na Issa Abdalah
Mgambo JKT: Godso nMmasa, Salum Mlima, Salim Gillah Ramadhani Malima, Novart Lufunga, Mohamed Samata, Salum Kipaga, Ally Nassoro, Fully Maganga, Malimi Busungu na Abuu Agoe
Kwenye benchi: Said Lubawa, Ayoub Salehe, Sabri Makame, Nassoro Gumbo, Mohamed Mustafa na Ramadhani Pera
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni