YANGA SC itamenyana na Azam FC katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hiyo inafuatia ushindi wa bao 1-0 jioni ya leo dhidi ya Khartoum N ya Sudan katika mchezo wa mwisho wa Kundi A Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na kwa matokeo hayo, Yanga SC inamaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi hilo kwa pointi zake tisa, baada ya kushinda mechi tatu, zikiwemo dhidi ya KMKM ya Zanzibar 2-0 na Telecom ya Djibouti 3-0.
Bao hilo pekee la Yanga SC leo limefungwa na mshambuliaji wake wa kimataifa wa Burundi, Amisi Joselyn Tambwe dakika ya 30 akimalizia kwa kichwa kona iliyochongwa na Nahodha Haruna Niyonzima kutoka Rwanda dakika ya 30.
Sifa za kipekee zimuendee kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ aliyeokoa michomo mingi ya hatari langoni mwake hadi Yanga SC kuulinda ushindi huo.
Safu ya ulinzi ya Khartoum yenye mabeki warefu ilikuwa kikwazo cha mashambulizi ya mipira mirefu kutoka pembeni ya Yanga, kwani waliicheza kwa wingi na kuiondosha katika hatari.
Yanga SC inamaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Gor Mahia ya Kenya yenye pointi 10, wakati Khartoum kwa pointi zake saba inamaliza nafasi ya tatu, ingawa nayo imefuzu Robo Fainali.
Robo Fainali za kwanza zinatarajiwa kuchezwa Jumanne kati ya APR ya Rwanda na Khartoum N na Gor Mahia na Malakia ya Sudan Kusini, wakati za pili zitachezwa Jumatano kati ya Al Shandy ya Sudan na KCCA ya Uganda na baadaye, Yanga SC na Azam FC zote za Dar es Salaam.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa, Jopseph Zutah, Oscar Joshua/Mwinyi Hajji Mngwali dk46, Pato Ngonyani, Kevin Yondani/Nadir Haroub ‘Cannavro’ dk83, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Haruna Nyonzima, Amisi Tambwe, Malimi Busungu na Andrew Coutinho/Godfrey Mwashiuya dk65.
Khartoum N; Mohamed Ibrahim, Amin Ibrahim, Hamza Daoud, Salaheldin Mahamoud, Samawal Merghani, Wagdi Awad, Antony Akumu Agay, Domenic Abui, Atif Khalif/Ismail Baba dk46, Badreldin Eldoon/Marwan Salah dk62 na
Ahmed Adam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni