MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC wamepeleka salamu Unguja, ambako wapinzani wao katika mechi ya Ngao ya Jamii, Azam FC wameweka kambi
Yanga SC leo imeichapa mabao 3-2 timu ngumu, Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini MBEYA katika mchezo wa kirafiki, ikiwa ni wiki moja kabla ya kukutana na Azam FC katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
Wenyeji, Mbeya City ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya nane kupitia kwa Bakari Mwinjuma baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Yanga.
Yanga SC walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 16 kupitia kwa Mbrazil Andrey Coutinho aliyemalizia krosi ya Mzimbabwe, Donald Ngoma.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Tambwe akaifungia Yanga SC bao la pili dakika ya 45 akimalizia tena kroi ya Ngoma.
Dakika mbili tu baada ya kuanza kipindi cha pili, Yanga SC walifanikiwa kupata bao la tatu lililofungwa na Ngoma, aliyemalizia krosi ya Simon Msuva.
Mbeya City walifanikiwa kupata bao la pili dakika ya 83 kupitia kwa Meshack Ilemi aliyefumua shuti kali lililowapita mabeki wa Yanga SC na kipa wao, Ally Mustafa ‘Barthez’.
Yanga SC itaendelea na kambi yake ya Tukuyu mjini humo hadi hapo itaporejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa Ngao Agosti 22.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Aly Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Vincent Bossou/Mbuyu Twite dk46, Thabani Kamusoko, Simon Msuva/Deus Kaseke dk64, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe/Malimi Busungu dk67, Donald Ngoma/Sadi Juma dk70 na Andrew Coutinho/Godfrey Mwashiuya dk46.
Mbeya City; Hanington Kalyesubula, Kabanda John/Haroun Shamte dk68, Hassan Mwasapili, Rajab Seif/Christian Sembuli dk49, Juma Nyosso, Steven Mazanda, Hassan Selemani/Richard Peter dk68, Daud Raphael, Themi Felix/Geoffrey Mlawa dk62, Bakari Slang na Joseph Mahundi/Meshack Ilemi dk56.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni